SAKATA LA STAND YA KANGE LACHUKUA SURA MPYA, TABOA, TNCC NA JWT WAPINGA MPANGO WA KUBADILI MATUMIZI YA TERMINAL
Na Hadija Bagasha | TANGA
SAKATA la matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange mkoani Tanga limechukua sura mpya baada ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC) na Jumuiya ya Wafanyabiashara Wadogo Tanzania (JWT) kupinga madai kwamba wamiliki wa mabasi wamekataa kutumia kituo hicho.
Badala yake, taasisi hizo zimesema hazina pingamizi la kutumia terminal ya Kange, bali zinataka Serikali na Halmashauri ya Jiji la Tanga kutoa kipindi cha mpito cha miezi sita ili kukamilisha maboresho ya kituo hicho kabla ya mabasi yote kuhamishiwa kuanzia safari zake hapo.
Msimamo huo ulitolewa leo mbele ya waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya Meya wa Jiji la Tanga, Selebos Mustafa, kunukuliwa akisema Kamati ya Fedha ya Baraza la Madiwani imependekeza kubadili matumizi ya Kituo Kikuu cha Kange na kukifanya eneo la maegesho ya malori kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hakitumiki ipasavyo.
Viongozi wa TABOA, TNCC na JWT walisisitiza kuwa mabasi yaendayo mikoani yamekuwa yakipitia kituo hicho kila siku kwa ajili ya ukaguzi wa Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), pamoja na kulipia tozo zote zinazotakiwa, hivyo madai kwamba wamekigomea kituo hicho hayana msingi.
Makamu Mwenyekiti wa TABOA Mkoa wa Tanga, Albert Peter, alisema taarifa za kubadilishwa kwa matumizi ya kituo hicho zimeleta taharuki kwa wamiliki wa mabasi na wananchi, ilhali hawajawahi kukataa kukitumia.
Alisema changamoto kubwa ni kukosekana kwa huduma muhimu zinazohitajika katika terminal hiyo, ikiwemo sehemu za kukaa abiria, kituo cha huduma ya kwanza, kituo cha polisi na miundombinu bora ya daladala kwa ajili ya usafiri wa kuunganisha wasafiri.
"Tulikaa na uongozi wa Halmashauri na kuomba maboresho hayo yafanyike, lakini hadi sasa hayajatekelezwa. Tunaamini mazingira yakiboreshwa, kituo kitakuwa rafiki kwa abiria na waendeshaji wa mabasi," alisema Albert.
Kwa upande wake, Meneja wa TNCC Mkoa wa Tanga, Charles Hoza, alisema taasisi hiyo imeamua kuingilia kati baada ya kupokea maombi kutoka TABOA na JWT kwa lengo la kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo badala ya maamuzi ya upande mmoja.
Naye Naibu Katibu wa TABOA Mkoa wa Tanga, Hassan Hashim, alisema chanzo cha sintofahamu ni uamuzi wa Halmashauri kupiga marufuku mabasi kupakia abiria katika terminal zao zilizopo katikati ya jiji na kuagiza safari zote zianzie Kange.
Alisisitiza kuwa TABOA haijawahi kupinga uamuzi huo kwa kuwa mabasi yao tayari hupitia Kange kwa ukaguzi wa Trafiki na LATRA pamoja na kulipa tozo zote kabla ya kuendelea na safari.
"Hatukatai kutumia Kange. Tunachosisitiza ni kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwanza ili abiria wapate mazingira bora ya kusafiria," alisema Hashim.
Katibu wa JWT Mkoa wa Tanga, Ismail Masoud, alisema baada ya mazungumzo kati ya wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi, wamekubaliana kuiomba Serikali kutoa kipindi cha mpito cha miezi sita.
Alisema ndani ya muda huo, Halmashauri ikamilishe maboresho ya terminal ya Kange huku wamiliki wa mabasi wasiokuwa na terminal zao wakijenga vituo vyao.
"Baada ya miezi sita, mabasi yote yatimize masharti yaliyowekwa. Wasiokuwa na terminal zao waanzie safari Kange, na atakayekiuka hatua za kisheria zichukuliwe," alisema.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Tanga, Selebos Mustafa, alisema awali Halmashauri, LATRA, Jeshi la Polisi na wamiliki wa mabasi walikubaliana mabasi yote yaendayo mikoani yaanzie safari Kange kuanzia Julai 15 mwaka huu, na hata matangazo rasmi yalitolewa kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema utekelezaji wa uamuzi huo ulisitishwa ghafla siku hiyo bila Halmashauri kushirikishwa, jambo lililosababisha sintofahamu na kuibua mjadala unaoendelea kuhusu hatima ya matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange.






Post a Comment