WANNE WAHUKUMIWA KUNYONGWA KWA MAUAJI YA MTOTO (13), MGANGA WA KIENYEJI MIONGONI MWAO
By Arushadigital|TABORA
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa watu wanne, akiwemo mganga wa kienyeji, baada ya kuwatia hatiani kwa mauaji ya kinyama ya msichana Kwangu Ngassa (13), mkazi wa Kijiji cha Ilula, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Katika hukumu hiyo, mahakama ilieleza kuwa washtakiwa hao walishirikiana kupanga na kutekeleza mauaji hayo ya kikatili, ambapo walimshambulia mtoto huyo kwa kumchoma kisu shingoni kabla ya kumkatakata sehemu zake za siri.
Tukio hilo lilitokea Januari 21, 2022 katika Kijiji cha Ilula na lilizua mshtuko mkubwa miongoni mwa wananchi kutokana na ukatili uliotumika dhidi ya mtoto huyo.
Baada ya uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola, watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa Mahakama Kuu kujibu shtaka la mauaji, ambapo ushahidi uliowasilishwa ulitosha kuwathibitishia hatia.
Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Majuto Lutema, Sida Mayeka, Kulwa Masunga na Idd Malaba, huku mahakama ikieleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi uliowaunganisha moja kwa moja na mauaji hayo.
Hukumu hiyo inahitimisha kesi iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne tangu kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha.

Post a Comment