Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
WANANCHI wa Arumeru Magharibi wameanza kunufaika na huduma za kibingwa za afya ya kinywa na meno baada ya madaktari bingwa kutoka Ujerumani kuanza rasmi ziara ya siku saba ya kutoa matibabu ya bure, elimu ya afya na kufanya utafiti kuhusu athari za magonjwa ya meno yanayochangiwa na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride kwenye maji.
Hatua hiyo inakuja wakati Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, akitimiza ahadi aliyowahi kuitoa kwa wananchi ya kuwaleta madaktari bingwa kutoka Ujerumani ili kusaidia kupunguza tatizo la magonjwa ya kinywa na meno ambalo limekuwa likiathiri wakazi wa maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Mpango huo unatekelezwa na Shirika la Ngorongoro Education Project Tanzania UK (NET) kwa kushirikiana na Dental Global ya Ujerumani, ukihusisha utoaji wa matibabu ya bure, mafunzo kwa wataalamu wa afya, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kati ya Tanzania na Ujerumani, pamoja na kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi wa NET, Engais Lukumay, alisema mpango huo umeanza Julai 20 na utaendelea kwa siku saba, ukilenga kuwafikia zaidi ya wananchi 1,500 kupitia huduma za uchunguzi, matibabu na elimu ya afya ya kinywa na meno.
Alisema timu hiyo inaongozwa na Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka Ujerumani, Dkt. Ursula Elizabeth, ambaye pia anatarajiwa kufanya utafiti wa kina kuhusu ukubwa wa tatizo la magonjwa ya meno nchini, hususan katika Arumeru Magharibi, ili kuweka msingi wa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Engais Lukumay, mbali na kliniki ya matibabu ya bure, wataalamu hao watatembelea shule, vituo vya watoto yatima na makundi maalumu ikiwemo watu wanaopambana na uraibu wa dawa za kulevya, wakitoa elimu ya afya ya kinywa na meno pamoja na huduma za matibabu.
Aidha, wanafunzi watakaofikiwa katika shule mbalimbali watagawiwa mishwaki na dawa za meno sambamba na kufundishwa namna sahihi ya kutunza afya ya kinywa na meno ili kujenga utamaduni wa kinga tangu wakiwa wadogo.
Alisema wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo makubwa ya meno watapatiwa rufaa na kupelekwa Hospitali ya Seliani katika siku mbili za mwisho za programu kwa ajili ya matibabu ya kibingwa.
"Programu hii imejengwa katika maeneo matatu makuu; kutoa elimu ya afya ya kinywa na meno, kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania na Ujerumani, na kutoa huduma za matibabu ya meno bila malipo kwa wananchi," alisema.
Mbali na huduma za sasa, alisema NET imeanza maandalizi ya kujenga kliniki ya kisasa ya afya ya kinywa na meno katika eneo la Ngaramtoni, ambayo itakuwa kituo cha kudumu cha huduma na mafunzo kwa wataalamu wa Tanzania na Ujerumani.
Alisema kliniki hiyo pia itakuwa kitovu cha mpango wa kubadilishana uzoefu (exchange programme), ambapo wanafunzi na madaktari wa Tanzania watapata nafasi ya kwenda Ujerumani kwa mafunzo ya vitendo, huku wataalamu wa Ujerumani wakija nchini kutoa huduma na kuwajengea uwezo wenzao wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, alisema ujio wa wataalamu hao ni utekelezaji wa ahadi aliyowapa wananchi na sehemu ya mkakati wa kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya magonjwa ya meno inayochangiwa na kiwango kikubwa cha fluoride kwenye maji.
"Niliahidi kuwaletea wananchi wetu madaktari bingwa wa afya ya kinywa na meno, na leo ahadi hiyo imetimia. Mbali na kutoa huduma, watafanya utafiti utakaotusaidia kufahamu ukubwa wa tatizo na kuweka msingi wa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta hii muhimu," alisema Dkt. Lukumay.
Alisema Dkt. Ursula Elizabeth ameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno kupitia uwekezaji, mafunzo kwa wataalamu wa ndani na tafiti zitakazosaidia kupata suluhisho la kudumu kwa athari za fluoride zinazowakabili wananchi wa Arumeru Magharibi.
Dkt. Lukumay alisema katika msafara huo madaktari wa Ujerumani wameambatana na madaktari wa Tanzania, hatua inayolenga kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani kupitia kubadilishana uzoefu wa kitaalamu.
Mbunge huyo alisema kuanza na wanafunzi ni hatua muhimu ya kujenga kizazi chenye uelewa wa kutunza afya ya kinywa na meno, akisisitiza kuwa kinga ndiyo silaha muhimu zaidi ya kupunguza magonjwa hayo katika jamii.
Alitoa wito kwa wananchi wa Arumeru Magharibi kujitokeza kwa wingi kutumia huduma zinazotolewa na timu hiyo ya madaktari, akisema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani utafungua ukurasa mpya wa kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini huku ukiweka msingi wa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta hiyo.
ENDS ..






















Post a Comment