SHULE 10 ZA SEKONDARI TANGA ZAINGIZWA KWENYE MPANGO MAALUM KUINUA UFAULU WA MITIHANI.
Na Hadija Bagasha Tanga,
Shule kumi za sekondari katika Jiji la Tanga ambazo zimekuwa zikirekodi matokeo duni katika mitihani ya taifa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi minne mfululizo zimeingizwa katika mpango maalum wa kuboresha ufaulu, unaolenga kuongeza kiwango cha mafanikio ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne pamoja na kubaini chanzo halisi cha changamoto zinazochangia matokeo hayo.
Shule zilizonufaika na mpango huo ni Nguvumali, Mikanjuni, Hoteni, Kihere, Mwapachu, Tongoni, Kirare, Marungu, Mabokweni pamoja na shule nyingine iliyochaguliwa chini ya tathmini ya mradi huo.
Mpango huo unatekelezwa na TangaYetu kwa ufadhili wa Botnar Foundation ya Uswisi kwa kushirikiana na taasisi ya Innovex na Tanzania Centre for Education, ukiwa na lengo la kuinua ubora wa elimu katika Jiji la Tanga kupitia mafunzo kwa wanafunzi, walimu na wadau wa elimu.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwapachu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education, Yusuph Ugutu, alisema shule hizo zilichaguliwa baada ya tathmini kubaini kuwa zimekuwa zikifanya vibaya katika mitihani ya taifa kwa miaka mitatu hadi minne mfululizo.
Alisema programu hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujifunza, mbinu za kujibu maswali ya mitihani na kuongeza ari ya kufanya vizuri, huku ikitoa fursa ya kubaini changamoto zinazokwamisha ufaulu.
"Lengo letu kubwa ni kuongeza kiwango cha ufaulu katika Jiji la Tanga kutokana na matokeo hafifu ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa miaka mitatu hadi minne mfululizo kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za NECTA. Sambamba na hilo tunaendelea na utafiti utakaotusaidia kubaini kwa kina sababu zinazochangia matokeo hayo ili tupate suluhisho la kudumu," alisema Ugutu.
Aliongeza kuwa mpango huo hautawalenga wanafunzi pekee, bali pia utahusisha walimu, maafisa elimu wa kata, maafisa wa Halmashauri ya Jiji la Tanga na wadau wengine wa elimu kupitia semina mbalimbali zitakazolenga kuboresha mbinu za ufundishaji na usimamizi wa elimu.
Kwa mujibu wa Ugutu, tathmini ya matokeo ya shule hizo imeonyesha kuwa baadhi yake zimekuwa zikikosa kabisa wanafunzi wanaopata Daraja la Kwanza, huku idadi ya wanaofaulu kwa Daraja la Pili ikiwa ndogo, hali iliyoifanya taasisi hiyo kuanzisha programu maalum ya kuokoa kiwango cha ufaulu.
"Tulipochambua matokeo tulibaini kuwa baadhi ya shule hazina kabisa wanafunzi wanaopata Daraja la Kwanza na hata Daraja la Pili ni wachache.
Hiyo ndiyo sababu iliyotusukuma kuanzisha mpango huu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Jiji la Tanga," alisema.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Kata ya Masiwani, Mohamed Khamis Matumbo, alisema mpango huo umekuja wakati muafaka kwani utawasaidia wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na kidato cha nne kuwa na maandalizi bora zaidi.
Alisema wanafunzi wengi hukumbwa na changamoto za lugha, uelewa wa maswali pamoja na mbinu za kujibu mitihani, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza kujiamini na kufanya vizuri.
"Mpango huu una manufaa makubwa kwa watoto wetu. Wengi wao hukosa alama nzuri si kwa kutosoma, bali kutokana na changamoto za kuelewa maswali na mbinu za kujibu mitihani. Kupitia mafunzo haya wamepata uelewa mpana wa namna ya kujibu maswali na kutambua kinachohitajika katika kila swali," alisema Matumbo.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walieleza kuwa programu hiyo imewapa matumaini mapya ya kuboresha matokeo yao, wakisema wamepata mbinu bora za kujifunza, kupanga muda wa masomo na kujibu maswali ya mitihani kwa ufanisi.
Walisema pia mafunzo yatakayotolewa kwa walimu yataongeza ubora wa ufundishaji darasani, jambo litakalosaidia kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.
Mwisho.

إرسال تعليق