MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI MZITO WA BILIONI 3 TYPA MALL-LEGANGA
Na Joseph Ngilisho | Arumeru
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 umetembelea na kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Jengo la Biashara la Typha Mall lililopo Leganga, Wilaya ya Arumeru, mradi unaotarajiwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kufungua fursa mpya za biashara katika eneo hilo.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, Mkurugenzi wa Typha Mall–Leganga, Absalom Pallangyo, alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2019 kwa lengo la kujenga kituo cha kisasa cha biashara kitakachohudumia wakazi wa Leganga, Usa River pamoja na wasafiri wanaotumia Barabara Kuu ya Arusha–Moshi.
Pallangyo alisema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 3 umefikia hatua za mwisho za ukamilishaji na unatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema Typha Mall imejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa na itakuwa na huduma mbalimbali zikiwemo maduka ya biashara kwa wafanyabiashara wa aina mbalimbali, supermarket ya kisasa, nafasi za kukodisha kwa taasisi za umma na binafsi, ofisi za benki na kampuni mbalimbali pamoja na maegesho ya magari yenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya wateja.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, mradi huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwa jamii kwa kuzalisha ajira 75 za muda wakati wa utekelezaji na ajira 20 za kudumu mara baada ya kuanza kwa shughuli za kibiashara.
Aidha, alisema uwekezaji huo utaongeza mapato ya Serikali na Halmashauri kupitia kodi, ushuru na tozo mbalimbali, huku ukichochea ukuaji wa biashara na kuifanya Leganga kuwa eneo lenye mvuto zaidi kwa wawekezaji.
“Mradi huu ni sehemu ya mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Pallangyo.
Alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha sekta binafsi kuwekeza na kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Baada ya kupokea taarifa ya mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, aliweka jiwe la msingi la Jengo la Biashara la Typha Mall na kupongeza uwekezaji huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wakazi wa Leganga na maeneo jirani.
Ends










إرسال تعليق