MWENGE WA UHURU KUMULIKA MIRADI SABA YA MAENDELEO YA SH, BILIONI 3.9 JIJINI ARUSHA,ALLY KIBA KUKESHA NA MWENGE FFU-MOROMBO

 Na Joseph Ngilisho |ARUSHA

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 unaoanza kesho (leo) kuangaza katika jiji la Arusha zitapitia na kukagua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya takribani Sh bilioni 3.9, inayolenga kuboresha huduma za kijamii, kukuza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ofisini kwake leo Jumatano julai 8,2026 , Mkude alisema miradi hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika eneo la Kimondorosi, ujenzi wa Shule mpya ya Murieti iliyojengwa kwa mfumo wa ghorofa katika eneo la Bondeni City, jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Moivaro, mradi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Arusha, mradi wa ufugaji wa kuku wa mayai unaoendeshwa na sekta binafsi pamoja na ujenzi wa barabara ya Giliki katika Kata ya Sakina.

Mkude alisema shule ya Morieti imejengwa kwa mfumo wa ghorofa ili kutumia vizuri eneo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa ardhi katika mazingira ya mjini.

Aidha, alisema Mwenge wa Uhuru utatembelea kikundi cha vijana cha MACRINS kilichopo Ngarenaro , ambacho kilinufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri na kuanzisha mradi wa kusindika chakula cha mifugo.

Alisema kikundi hicho ni mfano wa mafanikio ya uwezeshaji wa vijana na kinathibitisha kuwa ajira zinaweza kupatikana kupitia ujasiriamali badala ya kutegemea kuajiriwa serikalini pekee.

Mkude aliwahamasisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutumia fursa za mikopo inayotolewa kupitia halmashauri pamoja na taasisi za fedha kwa ushirikiano na Serikali ili kujiongezea kipato.

Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, alisema Jiji la Arusha linaendelea kufanya vizuri kwa kuhamasisha matumizi ya majiko na gesi safi, huku elimu hiyo ikianza kutolewa mashuleni ili kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutumia nishati salama tangu wakiwa wadogo.

Akizungumzia mradi wa barabara ya Giliki, Mkude alisema awali fedha zilizotengwa zilitosha kujenga kilomita 1.1 pekee kati ya kilomita 1.7 zinazohitajika, lakini Halmashauri ya Jiji la Arusha ilitoa fedha za ziada kukamilisha sehemu iliyobaki baada ya wananchi kuonesha ushirikiano mkubwa katika kuibua mradi huo.

Alisema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mkude alisema Mwenge wa Uhuru utapokewa rasmi Julai 9 katika Viwanja vya Magereza Kisongo kuanzia saa 1:30 asubuhi kabla ya kuanza mbio za kukagua miradi hiyo.

Aliongeza kuwa usiku kutakuwa na mkesha wa Mwenge katika viwanja vya FFU Mworombo, utakaoambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Ali Kiba na Juma Nature.


Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم