MWANG'ONDA AZINDUA MRADI WA MAJI WA SH. MILIONI 54 TINGATINGA-LONGIDO

 SERIKALI YASEMA MAZINGIRA RAFIKI YANAVUTIA WAWEKEZAJI KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Na Joseph Ngilisho |Longido

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang'onda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki yanayowavutia wawekezaji na wadau wa maendeleo kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwang'onda alitoa kauli hiyo Julai 5, 2026, wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 katika Kijiji cha Tingatinga, Wilaya ya Longido. Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 54 umefadhiliwa na wadau wa maendeleo From Heart 2 Hand, na unatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 1,986.

Alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha huduma za maji kwa kujenga miundombinu inayosogeza huduma karibu na makazi ya wananchi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani inayolenga kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

"Niwaombe wananchi wa Tingatinga na Wilaya ya Longido kutambua kuwa Mama Samia anawapenda sana. Ndiyo maana amekuwa akisisitiza amani na utulivu, kwa sababu penye amani ndipo maendeleo yanapostawi. Amani iliyopo imewavutia wadau wa maendeleo kuja kuwekeza na kujenga miradi kama huu wa maji. Tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ili aendelee kuwaletea maendeleo wananchi," alisema Mwang'onda.

Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kugharamia mradi huo, akieleza kuwa Serikali inathamini mchango wao katika kuharakisha maendeleo ya jamii na itaendelea kushirikiana nao ili kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido, Dkt. Stephene Kiulusu, alisema Longido ni wilaya yenye ukame mkubwa, lakini Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya maji na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 50 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 70 kwa sasa.

Dkt. Kiulusu alimshukuru Rais Samia kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusafirisha maji kutoka chanzo cha Mto Simba mkoani Kilimanjaro hadi Longido kwa umbali wa takribani kilomita 80, akisema hatua hiyo imekuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya maji katika wilaya hiyo.

Alisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea katika sekta ya maji unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yake, sambamba na kuboresha ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم