MBUNGE LUKUMAY AMLILIA MAREHEMU RAFAEL LUKUMAY,ATOA HOTUBA NZITO,AIFARIJI FAMILIA KUWA NA UVUMILIVU KATIKA KIPINDI HIKI KIGUMU

MBUNGE LUKUMAY AMLILIA MAREHEMU RAFAEL LUKUMAY,ATOA HOTUBA NZITO,AIFARIJI FAMILIA  KUWA NA UVUMILIVU KATIKA KIPINDI HIKI KIGUMU

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Mzee Rafael Lukumay, aliyefariki dunia Juni 28, 2026, akisisitiza umuhimu wa mshikamano, upendo na uvumilivu wakati wa maombolezo.


Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Ngateu, eneo la Azimio, na kuhudhuriwa na maelfu ya watu Dkt. Lukumay alisema msiba ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, lakini ni wakati unaohitaji familia na jamii kushikamana ili kuwapa nguvu waliofiwa.

"Ni kipindi kigumu kwa familia, ndugu na marafiki, lakini nawasihi muendelee kuwa na moyo wa subira na matumaini. Mungu ndiye mfariji wa kweli, na ninaamini atawapa nguvu za kuhimili majonzi haya," alisema Dkt. Lukumay.

Alieleza kuwa Marehemu Mzee Rafael Lukumay alikuwa mtu aliyejijengea heshima kubwa katika jamii kutokana na uchapakazi wake, uadilifu na mchango wake katika kukuza shughuli za biashara, hususan biashara ya nyama, iliyowanufaisha watu wengi ndani na nje ya Wilaya ya Arumeru.

Katika uhai wake, Mzee Rafael alikuwa mfanyabiashara mashuhuri wa nyama aliyemiliki mabucha kadhaa, huku akitoa ajira kwa wananchi wengi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa eneo hilo kupitia shughuli zake za kibiashara.

Dkt. Lukumay alisema kifo cha mzee huyo si pigo kwa familia pekee, bali pia kwa jamii nzima iliyofaidika na mchango wake, akibainisha kuwa kumbukumbu ya kazi zake njema itaendelea kuishi mioyoni mwa wengi.

Aliwataka wanafamilia kuendeleza misingi ya umoja, upendo na maadili mema aliyoyaacha marehemu ili kuhifadhi heshima na urithi wake.

Ibada ya mazishi ilifanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Ngateu, lililopo Kitongoji cha Kiranyi, Wilaya ya Arumeru, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini, wafanyabiashara, ndugu, jamaa na mamia ya waombolezaji waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.

Mzee Rafael Lukumay atakumbukwa kama mmoja wa wafanyabiashara walioacha alama ya mafanikio, bidii na huduma kwa jamii katika Wilaya ya Arumeru.










Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم