MBUNGE KOOLA NA MAKOI WAFUNGUA UKURASA MPYA WA USHIRIKIANO, WAZINDUA MITAMBO YA KUBORESHA BARABARA VUNJO NA MOSHI VIJIJINI

 MFANO WA KOOLA NA MAKOI WAFUNGUA UKURASA MPYA WA USHIRIKIANO, WAZINDUA MITAMBO YA KUBORESHA BARABARA VUNJO NA MOSHI VIJIJINI

Na Joseph Ngilisho- MOSHI 

Historia mpya ya ushirikiano wa maendeleo imeandikwa mkoani Kilimanjaro baada ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, kuzindua mitambo ya greda kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na uboreshaji wa barabara za ndani katika majimbo yao.

Uzinduzi huo uliofanyika Julai 14, 2026, umeelezwa kuwa ni mwanzo wa ushirikiano wa kipekee kati ya majimbo hayo mawili, ambao unalenga kuharakisha maendeleo ya wananchi kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Vunjo na Moshi Vijijini yana historia ya kuwa eneo moja kabla ya kugawanywa na kuwa majimbo mawili ya uchaguzi, lakini kwa miaka mingi viongozi wake wamekuwa wakitekeleza shughuli za maendeleo kila mmoja kivyake. Hata hivyo, hatua ya Koola na Makoi kufanya kazi kwa pamoja imeonekana kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa maendeleo unaolenga manufaa ya wananchi wa pande zote.

Ushirikiano huo unakuja baada ya wabunge hao kuanzisha mpango wa pamoja wa kugawa miche ya kahawa na parachichi kwa wananchi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na kuinua kipato cha kaya. Sasa wameelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya barabara, wakiamini kuwa barabara bora ni msingi wa ukuaji wa uchumi wa vijijini.

Kupatikana kwa mitambo hiyo kunatarajiwa kuharakisha matengenezo ya barabara bila kutegemea kwa kiwango kikubwa wakandarasi au taasisi nyingine, huku gharama za utekelezaji zikitarajiwa kupungua na kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma kwa haraka zaidi.

Aidha, barabara zitakazoboreshwa zinatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa kahawa na mazao mengine kwenda sokoni, kuongeza upatikanaji wa huduma za usafiri, kurahisisha wagonjwa kufika hospitalini na wanafunzi kufika shuleni hata wakati wa mvua.

Wadau wa maendeleo wamepongeza hatua ya kuundwa kwa Kamati Maalumu ya kusimamia matumizi na matengenezo ya mitambo hiyo, wakisema itasaidia kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.

Pia wametoa wito kwa Watanzania waishio nje ya nchi wenye asili ya Vunjo na Moshi Vijijini kushiriki kuchangia maendeleo ya maeneo yao kupitia kusaidia uendeshaji na matengenezo ya mitambo hiyo.

Wakati huohuo, viongozi na wadau mbalimbali wamezitaka halmashauri na majimbo mengine nchini kuiga mfano wa ushirikiano ulioanzishwa na Mbunge wa Vunjo, Enock Zadock Koola, na Mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi, wakieleza kuwa mshikamano wa viongozi unaweza kuwa chachu ya kuharakisha maendeleo ya wananchi na uchumi wa maeneo yao.

Ends .

Post a Comment

أحدث أقدم