MBUNGE GIDO AWA KIVUTIO ZIARA YA MWENGE JIJI LA ARUSHA, APONGEZA MIRADI YA SAMIA YA MAJI, BARABARA NA ELIMU
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Marirtha Gido, ameibuka kuwa mmoja wa viongozi waliovutia zaidi katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 jijini Arusha baada ya kushiriki kikamilifu katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuwakilisha wabunge wenzake katika shughuli mbalimbali za Mwenge.
Katika ziara hiyo, Gido alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi wa Jiji la Arusha.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya zege ya Giriki yenye urefu wa kilomita 1.1, iliyozinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, Gido alisema miradi hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za msingi na kuinua uchumi wa wananchi.
Mbali na barabara hiyo, Gido aliipongeza Serikali kwa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika Mtaa wa Kimindorosi, Kata ya Olasiti, akieleza kuwa mradi huo utaleta mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.
Alisema wanawake wa Kimindorosi ndio watanufaika zaidi na mradi huo kwani utaondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hivyo kuwawezesha kutumia muda mwingi zaidi katika shughuli za uzalishaji mali, malezi ya familia na maendeleo ya kiuchumi.
"Miradi kama hii inaonyesha namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyojikita katika kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja. Hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa Arusha, hususan wanawake," alisema Gido.
Katika sekta ya elimu, Mbunge huyo aliisifu Serikali baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa katika Shule Mpya ya Sekondari Bondeni City, akisema uwekezaji huo utaongeza fursa za elimu bora kwa vijana wa Arusha.
Alieleza kuwa ujenzi wa shule hiyo utasaidia kuongeza idadi ya madarasa, kupunguza msongamano wa wanafunzi, kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
"Serikali inaendelea kuthibitisha kuwa inaamini elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa. Huu ni uwekezaji wa kizazi cha sasa na kijacho, kwani watoto wetu watapata mazingira bora ya kujifunza na kujiandaa kulijenga Taifa," alisema.
Gido alihitimisha kwa kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuelekeza rasilimali katika miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu, maji na elimu ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu ya Jiji la Arusha na Tanzania kwa ujumla.
..Ends...



Post a Comment