HILLARY MOLLEL: BARABARA YA ZEGE SAKINA NI ZAWADI YA RAIS SAMIA KWA WANANCHI

HILLARY MOLLEL: BARABARA YA ZEGE SAKINA NI ZAWADI YA RAIS SAMIA KWA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Diwani wa Kata ya Sakina, Hillary Mollel, amesema ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilomita 1.5 unaotekelezwa katika kata hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo itakayobadili maisha ya wananchi kwa kuboresha usafiri, kuchochea biashara na kuongeza thamani ya eneo hilo.



Akizungumza Julai 9, 2026, wakati Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 alipoweka jiwe la msingi la mradi huo, Mollel alisema wananchi wa Sakina wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo muhimu.

Alisema ujio wa Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi la barabara hiyo ni heshima kubwa kwa Kata ya Sakina na uthibitisho kuwa Serikali inaendelea kupeleka maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi.

"Barabara hii ni ya kimkakati. Ipo umbali mfupi kutoka katikati ya Jiji la Arusha na imekuwa ikihitajika kwa muda mrefu. Kukamilika kwake kutawanufaisha wakazi wa Sakina pamoja na wananchi kutoka maeneo jirani wanaoitumia kila siku," alisema Mollel.

Alifafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Halmashauri ya Jiji la Arusha, jambo linaloonyesha dhamira ya serikali ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya mijini kwa manufaa ya wananchi.

Mollel pia alimpongeza Mbunge wa Arusha Mjini ambaye ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, akisema ushirikiano kati ya viongozi umewezesha ndoto ya wananchi wa Sakina kuanza kutimia.

Aidha, aliwapongeza wananchi wa Kata ya Sakina kwa kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru na kuunga mkono miradi ya maendeleo.

"Ushiriki wenu umeonyesha umoja na uzalendo wa hali ya juu. Sakina imeandika historia kwa mapokezi makubwa ya Mwenge wa Uhuru. Tuendelee kushikamana katika kusimamia miradi ya maendeleo na kujenga jamii yenye mshikamano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema Mollel.






Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post