MAMA AWAFUNGIA NDANI NA KUWACHOMA MOTO WATOTO WAKE

 MAMA ADAIWA KUWAFUNGIA WATOTO WAWILI NDANI, AWAUNGUZA KWA MOTO KENYA

Na Arushadigital|KENYA

Hali ya majonzi imetanda katika Kijiji cha Sosik, Kaunti ya Bomet nchini Kenya, baada ya mama mmoja kudaiwa kuwafungia watoto wake wawili wadogo ndani ya nyumba kisha kuichoma moto, tukio lililosababisha vifo vya watoto hao.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Sotik, Sammy Choge, alisema mshukiwa huyo, Brenda Chelangat Cheruiyot (40), anadaiwa kurejea nyumbani usiku wa kuamkia leo na kuwakuta watoto wake wawili, Enock Kiptoo (3) na Aron Kipkirui (6), wakiwa ndani ya nyumba.

Kwa mujibu wa polisi, mama huyo alifunga mlango wa nyumba kutoka nje kabla ya kuwasha moto na kutoroka eneo la tukio.

Majirani waliosikia vilio vya watoto na kuona nyumba ikiteketea walikimbilia kutoa msaada, lakini juhudi zao hazikufanikiwa kutokana na moto kusambaa kwa kasi na kuifunika nyumba nzima.

Baada ya tukio hilo, wakazi wenye hasira walimfuatilia mshukiwa na kudaiwa kujaribu kumshambulia, lakini polisi waliwasili kwa wakati na kumwokoa kabla ya kumkamata.

Mshukiwa kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Ndanai huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo lililowaacha wakazi wa eneo hilo katika simanz kubwa.

Post a Comment

أحدث أقدم