MADAKTARI WA UJERUMANI WAFICHUA UKUBWA WA TATIZO LA MENO ARUMERU,HOSPITALI YA SELIANI -NGARAMTONI YAMPONGEZA MBUNGE LUKUMAY

MADAKTARI WA UJERUMANI WAFICHUA UKUBWA WA TATIZO LA MENO ARUMERU

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

ZIARA ya madaktari bingwa wa kinywa na meno kutoka Ujerumani imeibua ukubwa wa changamoto ya afya ya meno kwa watoto wa shule na wananchi wa Arumeru, hali iliyozua mpango wa kuanzishwa kwa ushirikiano wa muda mrefu wa kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno nchini.

Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, alisema matokeo ya uchunguzi wa awali uliofanywa na timu ya wataalamu kutoka Tanzania na Ujerumani yameonesha hitaji la haraka la kuwekeza katika kinga, tiba na wataalamu wa afya ya meno.

Akizungumza jana katika Hospitali ya Selian-Ngaramtoni baada ya kutembelea kambi ya matibabu ya bure ya meno, Dkt. Lukumay alisema changamoto iliyobainika imewashawishi wadau wa kimataifa kubadili mipango yao na kuanza kusaidia kuimarisha huduma nchini badala ya kuajiri madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi Ujerumani.

"Walikuja wakitarajia kuajiri madaktari wa meno 100 kutoka Tanzania. Lakini baada ya kuona ukubwa wa changamoto tuliyonayo, wameamua kwanza tushirikiane kujenga uwezo wa huduma hapa nchini," alisema.

Alisema ushirikiano huo utatekelezwa kupitia Dental Global ya Ujerumani kwa kushirikiana na NEPT-UK Tanzania na taasisi nyingine, ukijumuisha matibabu ya kibingwa, mafunzo kwa madaktari wa Tanzania, kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za afya ya meno kwa muda mrefu.

Dkt. Lukumay alisema madaktari hao wakiongozwa na Dkt. Ursula Suessbier pia wamevutiwa na kiwango cha uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya baada ya kukuta vifaa vya kisasa vya matibabu ya meno vinavyofanana na vinavyotumika nchini Ujerumani.

"Hii inaonyesha dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya na kujenga mazingira yanayowezesha ushirikiano wa kimataifa," alisema.

Mbunge huyo alisema mafanikio hayo yamechangiwa na sera ya diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa inayoiwezesha Tanzania kuvutia wataalamu na washirika wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali.

Aliongeza kuwa ataendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka Ujerumani, Uingereza na Hispania kutafuta rasilimali za kutekeleza miradi ya afya, maji na elimu, hususan katika maeneo yanayoathiriwa na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Selian-Ngaramtoni, Dkt. Amon Marti, alisema ujio wa madaktari hao umefungua ukurasa mpya wa kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno katika hospitali hiyo.

Alisema mamia ya wananchi wamehudumiwa katika kambi hiyo, huku wataalamu wa hospitali wakinufaika kwa kubadilishana ujuzi na uzoefu na madaktari kutoka Ujerumani.

Dkt. Marti alisema tathmini ya awali imeonesha kuwa magonjwa ya kinywa na meno bado ni changamoto kubwa kwa watoto na jamii katika Arumeru, jambo linalohitaji uwekezaji zaidi katika vifaa tiba, elimu ya afya na kuongeza wataalamu wa meno.

"Huu si ushirikiano wa siku chache, bali ni mwanzo wa safari ya kuboresha huduma za afya ya meno kwa wananchi wetu," alisema.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم