LUKUMAY AMPONGEZA RAIS SAMIA, AIBUA KERO ZA UMEME MJI MDOGO WA NGARAMTONI NA MIKOPO YA ASILIMIA 10
Na Joseph Ngilisho-ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, miundombinu na huduma za kijamii, huku akiitaka kuongeza kasi ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC).
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Julay 01,2026 kilichojadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Dkt. Lukumay alisema serikali imeendelea kuonyesha dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo Watanzania kupitia uwekezaji mkubwa katika elimu, ikiwemo utoaji wa elimu bila malipo na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Alisema serikali pia imeendelea kujenga shule za kisasa na kuboresha miundombinu ya elimu, hatua ambazo zimeongeza fursa za watoto wengi kupata elimu bora.
Akizungumzia huduma za umeme, Dkt. Lukumay alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kupitia miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, bado wananchi wa Mji Mdogo wa Ngaramtoni wanakabiliwa na changamoto ya kutofikiwa kikamilifu na huduma hiyo muhimu.
Aliiomba serikali kupitia Wizara ya Nishati na taasisi zake kuhakikisha maeneo yaliyosalia ndani ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni yanaunganishwa na huduma ya umeme kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika na shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mbunge huyo pia alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ushirikiano wake na viongozi mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Aidha, aliwataka madiwani kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utaratibu wa ukusanyaji wa mapato na tozo mbalimbali ili kuondoa malalamiko yanayotokana na kutofahamu viwango vinavyotakiwa kulipwa.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, Dkt. Lukumay alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kunufaika kikamilifu na fedha hizo.
Alikumbusha kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa serikali, asilimia nne ya fedha hizo hutengwa kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Alihitimisha kwa kuwataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za wananchi na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo chanya kwa wakazi wa Arumeru Magharibi na wilaya kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, aliwataka madiwani wa Halmashauri hiyo kuongoza kampeni ya usafi wa mazingira katika kata na vijiji vyao ili kulinda hadhi ya Wilaya ya Arumeru kama lango la Mkoa wa Arusha na kuzuia milipuko ya magonjwa.
Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Arusha DC kwa hatua ya kuanzisha mradi wa dampo la kisasa la kuhifadhi taka, huku Mwenyekiti wa Halmashauri, Baraka Simon Mesiaki, akiahidi madiwani wataongoza kampeni ya kuhamasisha usafi katika maeneo yao.
***Ends***






Post a Comment