GIDO AIBANA SERIKALI KUBUSU CHANGAMOTO YA BARABARA NA MAJI ARUMERU
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Martha Gido, ameitaka Serikali kupitia wizara na taasisi husika kuongeza kasi ya kutatua changamoto za miundombinu ya barabara na upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Arumeru, akisema matatizo hayo yanaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Gido alitoa wito huo alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, katika ziara ya Waziri wa Kilimo , Daniel Chongolo Mkoani Arusha.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi, viongozi wa chama na Serikali, alisema pamoja na Arumeru kuwa moja ya wilaya zinazotegemea zaidi kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wake, bado wakulima wanakabiliwa na changamoto ya barabara zisizokuwa katika hali nzuri, jambo linalochelewesha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni.
Alieleza kuwa ubovu wa barabara unasababisha gharama za usafirishaji kuongezeka, kupunguza thamani ya mazao na wakati mwingine kusababisha mazao kuharibika kabla hayajawafikia wanunuzi, hali inayowarudisha nyuma wakulima licha ya juhudi kubwa wanazoweka katika uzalishaji.
"Arumeru ina wananchi wachapakazi wanaotegemea kilimo kwa maisha yao, lakini maendeleo yao yanakwamishwa na miundombinu duni ya barabara. Tunaomba Serikali ipe eneo hili kipaumbele ili wakulima wetu waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuongeza kipato chao," alisema Gido.
Mbali na barabara, mbunge huyo alisema upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto inayowaathiri wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, akibainisha kuwa miradi ya maji ya Sampu, Mbaseni, Msamaria na Madiachai imechukua muda mrefu kukamilika.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutamaliza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa matumizi ya nyumbani, mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha, alisisitiza kuwa wanawake na watoto wa kike ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa tatizo la maji, kwani hutumia muda mwingi kuyatafuta badala ya kushiriki kikamilifu katika uzalishaji, biashara na masomo.
Aliitaka Serikali kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji safi na salama, hatua ambayo alisema itachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Arumeru.
Katika mkutano huo, Gido pia alitoa salamu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa wananchi wa Arumeru wanatambua juhudi za Serikali katika kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Alimwomba Waziri Chongolo kufikisha salamu hizo kwa Rais, huku akisisitiza kuwa wananchi wa Arumeru wanaendelea kuiunga mkono Serikali na wana matumaini kuwa changamoto za barabara na maji zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kufungua fursa zaidi za maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Ends

إرسال تعليق