GASTON AMPONGEZA SAMIA KWA MAPINDUZI YA SEKTA YA UTALII
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Space East Afrika LTD, inayojihusisha na uwekezaji katika sekta ya utalii na umiliki wa hoteli za kitalii Serengeti, Gaston Francis, amewataka Watanzania kujitokeza kuwekeza katika sekta ya utalii, akisisitiza kuwa fursa zilizopo si za wawekezaji wa kigeni pekee bali ni za wananchi wote.
"Taasisi zina mifumo yake ya uendeshaji. Viongozi wanabadilishana vijiti lakini taasisi zinaendelea kusimamia ajenda za serikali. Kiongozi anayekuja anatakiwa kuendeleza mafanikio yaliyopo na kufungua fursa mpya kwa maendeleo ya taifa," alisema.
Francis alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeifanya sekta ya utalii kupiga hatua kubwa kupitia sera na mikakati iliyoongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania mwaka mzima.
Alisema tofauti na ilivyokuwa awali ambapo utalii ulikuwa na misimu maalumu, kwa sasa hifadhi nyingi, ikiwemo Serengeti, zinaendelea kupokea watalii karibu kipindi chote cha mwaka kutokana na mafanikio ya kampeni na maboresho yaliyofanywa na serikali.
"Leo hii hakuna tena dhana ya msimu wa watalii kama ilivyokuwa zamani. Wageni wanaendelea kuja kwa wingi na hiyo ni fursa kubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje," alisema.
Alibainisha kuwa ongezeko hilo la watalii limeongeza mahitaji ya huduma za malazi na uwekezaji mwingine katika sekta hiyo, hali inayoonyesha kuwa juhudi za serikali zimeanza kuzaa matunda makubwa.
Aidha, aliwataka Watanzania kuondoa dhana kwamba uwekezaji katika utalii ni wa wageni pekee, akisema bado kuna hifadhi nyingi zenye fursa kubwa ambazo hazijatumika ipasavyo.
"Watanzania tufike katika ofisi za mamlaka za utalii, tupate elimu na taarifa kuhusu fursa zilizopo. Uwekezaji wa utalii si wa wazungu pekee; ni wetu sote na tuna kila sababu ya kutumia nafasi hii kuinufaisha nchi na familia zetu," alisema.
Francis pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuifungua sekta ya utalii, akisema mafanikio yanayoonekana sasa, yakiwemo ongezeko la watalii na uhitaji mkubwa wa maeneo ya malazi, ni ushahidi wa utekelezaji mzuri wa sera za serikali.
"Hakuna anayebisha kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika sekta ya utalii. Mbuga zimefunguka zaidi, watalii wameongezeka na sasa changamoto kubwa ni kuongeza huduma za kuwahudumia wageni. Hii ni ishara kuwa malengo ya serikali yamevukwa," alisema.
Alimtakia mafanikio Kamishna mpya wa TANAPA, Massana Mwishawa, akieleza kuwa anaingia katika kipindi ambacho sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kasi, hivyo ana wajibu wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha ushirikiano kati ya TANAPA, sekta binafsi na wadau wengine wa utalii.
Aidha, aliwataka wadau wa utalii kuendelea kushirikiana na serikali katika kutangaza vivutio vya utalii na kuwekeza zaidi kwenye huduma mbalimbali ili Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kuvutia watalii.
**Ends ***



إرسال تعليق