DKT. LUKUMAY: SAMIA ALETA MAPINDUZI YA MAENDELEO ARUSHA DC
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali umebadili sura ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na kuongeza fursa za ajira, elimu, afya na miundombinu.
Akizungumza baada ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 kupita wilayani humo leo Ijumaa Julai 10,2026, Dkt. Lukumay alisema Mwenge umezindua miradi mitano na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi miwili yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.7, hatua aliyoieleza kuwa ushahidi wa dhamira ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema moja ya miradi iliyomvutia zaidi ni uwekezaji wa sekta binafsi katika mradi wa nishati, ambao umefungua nafasi za ajira kwa zaidi ya wananchi 100, sambamba na miradi ya ofisi za kata na shule za sekondari zinazoongeza huduma kwa wananchi.
"Shule ya Sekondari Kiutu ni mfano wa uwekezaji unaolenga kuimarisha elimu ya sayansi. Ina maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia ambazo zinawawezesha wanafunzi kufanya mafunzo ya vitendo na kutimiza azma ya Serikali ya kuongeza wataalamu wa sayansi nchini," alisema.
Mbunge huyo alisema wananchi wameonesha imani kubwa kwa Rais Samia kutokana na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayogusa maisha yao ya kila siku.
Aidha, alimpongeza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, kwa kutumia mbio hizo kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya, pamoja na kuhimiza uwajibikaji katika sekta za elimu, afya na miundombinu.
Katika miundombinu, Dkt. Lukumay alisema daraja la Seliani limekuwa mkombozi kwa wananchi wa kata za Olorien na Tarakwa kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao ya mbogamboga kwenda Soko la Ngaramtoni na kuwawezesha wanafunzi kufika shuleni kwa urahisi.
Akizungumzia mafanikio ya Serikali kwa ujumla, alisema katika sekta ya afya Rais Samia ameendelea kuimarisha huduma za afya msingi kwa kujenga hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini, hatua iliyopanua upatikanaji wa huduma karibu na wananchi.
Alisema katika elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, huku bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ikiongezwa na kuwawezesha mamia ya maelfu ya wanafunzi kuendelea na masomo yao.
Kwa upande wa maji, alisema utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaendelea, huku Serikali ikitoa zaidi ya Sh bilioni 2.7 kwa ajili ya kusambaza maji katika kata mbalimbali kupitia mradi mkubwa wa maji wa Arusha.
Dkt. Lukumay alisema mafanikio hayo yanatokana na uchumi kuendelea kuimarika, hali inayowezesha Serikali kugharamia miradi mingi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani.
Aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili utekelezaji wa miradi ya maendeleo uendelee kuwafikia Watanzania wote.
Ends.






Post a Comment