BARABARA YA KM 28 YA LAMI MERU YAANZA KWA KISHINDO, MWENGE WATEMBELEA MRADI WA SH BILIONI 5.2

 Na Joseph Ngilisho | ARUMERU 

WANANCHI wa Wilaya ya Meru wanatarajia kunufaika na mageuzi makubwa ya miundombinu baada ya Mbunge wa Arumeru Magharibi, Joshua Nassari, kutangaza kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa barabara ya kilomita 28 kwa kiwango cha lami.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang'onda, amekagua na kuweka jiwe la msingi la mradi mwingine wa barabara ya Tengeru–Nambala unaotekelezwa kwa zaidi ya Sh bilioni 5.2.


Akizungumza wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Meru, Nassari alisema tayari zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mererani–Mbuguni–Usa River yenye urefu wa kilomita 28 imetangazwa, hatua inayofungua njia ya kumpata mkandarasi na kuanza utekelezaji wa mradi ambao wananchi wameusubiri kwa muda mrefu.

"Hii ni habari njema kwa wananchi wa Meru. Ndani ya siku chache zijazo tutaanza kuona hatua za utekelezaji wa mradi huu muhimu ambao wananchi wameusubiri kwa muda mrefu," alisema Nassari.

Alisema uwekezaji huo unaongezea mafanikio ambayo tayari yanaonekana katika sekta mbalimbali za maendeleo wilayani humo, ikiwemo afya ambapo Serikali imejenga jengo la kisasa la radiolojia katika Hospitali ya Halmashauri ya Meru pamoja na kutoa Sh milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika Kata ya Kikwe.

Mbunge huyo alisema miradi ya barabara, afya, elimu na maji inaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wa Meru.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tengeru–Nambala yenye urefu wa kilomita 3.8 unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa gharama ya jumla ya Sh bilioni 5.2 kupitia awamu nne.

Taarifa iliyowasilishwa na Meneja wa TARURA Arumeru, Mhandisi Julius Kaaya, ilieleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mita 500 kwa kiwango cha lami imekamilika kwa asilimia 100, huku awamu ya pili ya mita 700 inayotekelezwa na kampuni ya Rocktronic Limited ikiwa imefikia asilimia 54 na inatarajiwa kukamilika Septemba 3, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi huo utarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda masokoni, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii, kupunguza gharama za usafiri, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Tarafa za Poli, Mbuguni na maeneo jirani.

Nassari aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda miradi ya maendeleo ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo, akisisitiza kuwa Meru inaendelea kufungua ukurasa mpya wa maendeleo kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta za kimkakati.


Ends..

.

Post a Comment

Previous Post Next Post