DKT LUKUMAY AANIKA MAFANIKIO MAKUBWA YA CCM,AMPONGEZA RAIS SAMIA ATAKA CCM ISIMAMIE SERIKALI KWA VITENDO ILI WANANCHI WAENDELEE KUKIAMINI


CCM: TUSIMAMIE SERIKALI KWA VITENDO ILI WANANCHI WAENDELEE KUTUAMINI

Na Joseph Ngilisho | Arusha

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema jukumu kubwa la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa si kutangaza mafanikio ya Serikali kwa maneno, bali kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na miradi ya maendeleo unawafikia wananchi kwa ubora unaostahili ili kuendeleza imani yao kwa chama hicho.

Dkt. Lukumay alitoa kauli hiyo katika kikao maalum cha tathmini cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha kilichofanyika katika Makao Makuu ya CCM Mkoa huo, akisema tathmini imeonesha chama kinaendelea kuwa imara, lakini viongozi wake wanapaswa kuongeza nguvu katika kuisimamia Serikali ili wananchi waone matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema usimamizi wa karibu wa chama ndiyo utakaohakikisha fedha za umma na miradi ya maendeleo inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

"Chama kikisimamia Serikali vizuri, wananchi wataendelea kukiamini na kukipa ridhaa. Tunapaswa kuhakikisha kila mradi na kila fedha inayotolewa na Serikali inaleta matokeo kwa wananchi," alisema.

Alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta za afya na elimu yanahitaji kulindwa kwa usimamizi madhubuti wa viongozi wa CCM katika ngazi zote.

Kwa upande wa afya, alisema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwa kujenga hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 649 na zaidi ya zahanati 2700 nchini, huku jukumu la chama likiwa kuhakikisha wananchi wanapata dawa, wahudumu wa kutosha na huduma bora.

"Hatutaki majengo yabaki kuwa alama tu. Tunataka wananchi waingie kwenye vituo vya afya wakute dawa, wahudumu na huduma bora. Huo ndiyo usimamizi tunaoutaka," alisema.

Aliongeza kuwa katika sekta ya elimu, Serikali imeendelea kuimarisha elimu bila malipo, kujenga maelfu ya vyumba vya madarasa, kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuboresha stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu, hatua ambazo amesema zimeendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.

Dkt. Lukumay alisema wabunge wa CCM wataendelea kuisimamia Serikali kupitia utekelezaji wa bajeti na miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kama zilivyokusudiwa.

"Kazi yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, elimu, maji na miundombinu. Huo ndiyo msingi wa kuendelea kuijenga imani ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi," alisema.

Awali akifungua kikao hicho, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Rajabu Abdulrahman, alisema baada ya ushindi mkubwa wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, jukumu lililobaki sasa ni kuisimamia Serikali kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo ahadi zote zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030.

Rajabu alisema lengo la kikao hicho ni kuwakumbusha viongozi wa chama kuwa ushindi wa uchaguzi si mwisho wa safari, bali mwanzo wa wajibu mkubwa wa kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo waliyoyaahidiwa.

Alisema CCM ilifanikiwa kushinda uchaguzi kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kupata ushindi mkubwa wa wabunge na madiwani, hivyo viongozi wote wa chama wanapaswa kuhakikisha Serikali inatimiza ahadi zote ilizotoa kwa wananchi.

"Lengo la chama cha siasa ni kushika dola, na sisi tumefanikiwa. Lakini baada ya ushindi, kazi yetu kubwa sasa ni kuisimamia Serikali ili itekeleze yale yote tuliyowaahidi wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 hadi 2030," alisema.

Alisisitiza kuwa ilani ni mkataba kati ya CCM na wananchi, hivyo viongozi wa chama katika ngazi zote wanapaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, umeme, barabara na huduma nyingine muhimu.

"Kila kiongozi wa chama kwa nafasi yake lazima asimamie Serikali kwa vitendo. Wananchi walituamini kwa kutupa kura, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunaendeleza imani hiyo kwa kutekeleza yale yote tuliyowaahidi," alisisitiza.








Ends

Post a Comment

أحدث أقدم