BAKWATA YAANGUKIA PUA UMILIKI WA KIWANJA ARUSHA,MAHAKAMA YA RUFAA YATUPA MAOMBI YAO, MAJAJI WATATU WATHIBITISHA KUWA JUMUIYA YA WAISLAMU NDIO MMILIKI HALALI

 Na Joseph Ngilisho, Arusha

 

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imehitimisha mgogoro wa muda mrefu wa umiliki wa kiwanja kati ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Waislamu Mkoa wa Arusha (AMU), baada ya jopo la Majaji watatu kuthibitisha kuwa BAKWATA haikuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja kinachobishaniwa.

Hukumu hiyo ilitolewa jijini Arusha na jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Gerald Ndika, Omari Othuman Makungu na Mustafa Kambona Ismail, katika Rufaa ya Madai Na. 508 ya mwaka 2024, iliyotokana na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, katika Shauri la Ardhi Na. 29 la mwaka 2012.

Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, Jumuiya ya Waislamu Mkoa wa Arusha (AMU) iliwakilishwa na mawakili Median Mwale na Edmund Ngemela, huku upande wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ukiwakilishwa na Wakili Haruna Msangi.

Eneo na jengo lililokuwa likigombewa katikati ya jiji la Arusha

Kiini cha mgogoro huo ni umiliki wa Kiwanja Na. 34, Kitalu "G", Eneo "F", jijini Arusha, ambapo BAKWATA ilidai kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja hicho na kwamba AMU ilikimiliki na kukitumia bila kuwa na haki ya kisheria.

Kutokana na madai hayo, BAKWATA iliiomba Mahakama itangaze kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja hicho, iamuru AMU ikabidhi kiwanja hicho na kuacha kukitumia, pamoja na kutoa amri nyingine ambazo Mahakama ingeona zinafaa.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa na pande zote, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa BAKWATA haikufanikiwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo ikatupilia mbali shauri hilo.

BAKWATA ilikata rufaa katika Mahakama ya Rufani baada ya kutoridhika na uamuzi wa mahakama kuu ,ikidai kuwa Mahakama Kuu ilifanya makosa katika kutathmini ushahidi, ilipuuza baadhi ya vielelezo muhimu na kufikia hitimisho ambalo halikuendana na ushahidi uliowasilishwa.

Baada ya kupitia kwa kina hoja zote za rufaa, ushahidi uliowasilishwa na sheria zinazohusika, Majaji Gerald A.M. Ndika, Omari Othuman Makungu na Mustafa Kambona Ismail walibaini kuwa, ingawa baadhi ya sababu za rufaa zilikuwa na uzito na hivyo rufaa iliruhusiwa kwa sehemu, hali hiyo haikutosha kubadili hitimisho la msingi lililofikiwa na Mahakama Kuu.

Majaji hao walieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, mzigo wa kuthibitisha umiliki wa mali ulikuwa kwa mlalamikaji ambaye ni BAKWATA, lakini ushahidi uliowasilishwa haukuonyesha kwa kiwango kinachoridhisha kuwa ndiyo yenye haki ya kisheria ya kumiliki kiwanja hicho kuliko AMU.

Kwa msingi huo, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hitimisho la Mahakama Kuu kwamba BAKWATA haikuthibitisha madai yake ya umiliki wa kiwanja hicho, hivyo haikuona sababu ya kubadili uamuzi uliokuwa umetolewa awali.

Katika hitimisho lake, Mahakama iliamuru kila upande ujigharamie gharama zake mwenyewe za shauri, na hivyo kuhitimisha rasmi mgogoro huo wa muda mrefu uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Uamuzi huo unasisitiza kuwa katika mashauri ya umiliki wa ardhi, madai pekee hayatoshi, bali mhusika anayejidai kuwa mmiliki analazimika kuwasilisha ushahidi wa kutosha na wa kuaminika ili kuthibitisha haki yake mbele ya Mahakama.

Kwa upande wake Mustafa Kyago mwakilishi wa jumuiya ya waislamu (AMU) ,aliishukuru mahakama kwa kutenda haki  akidai imeonesha umma kwamba eneo hilo  ni mali halali ya jumuiya ya waislamu na ndo mwisho wa mgogoro huo uliochukua muda mrefu.

Ends. 

Post a Comment

أحدث أقدم