WAKILI FAUDHIA AWATAKA WANAWAKE KUTAMBUA NA KUTETEA HAKI ZAO
Na Arushadigital | ARUSHA
Wakili wa kujitegemea, Faudhia Mustapha, amewahimiza wanawake nchini kujifunza na kutambua haki zao za msingi zilizolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria mbalimbali ili waweze kujilinda dhidi ya ubaguzi, unyanyasaji na kunyimwa fursa za maendeleo.
Akizungumza katika jukwaa la KHANGA GALA lililofanyika jijini Arusha, Faudhia alisema wanawake wana haki sawa na wanaume katika nyanja zote za maisha na hawapaswi kubaguliwa kwa misingi ya jinsia.
Alieleza kuwa haki ya usawa na kutobaguliwa imeainishwa katika Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo zinatambua usawa wa watu wote mbele ya sheria.
“Wanawake na wanaume ni sawa mbele ya sheria. Hakuna anayepaswa kunyimwa haki au fursa kwa sababu tu ya kuwa mwanamke,” alisema.
Faudhia alisema haki nyingine muhimu kwa mwanamke ni haki ya kupata elimu, akibainisha kuwa elimu ndiyo msingi wa kuwawezesha wanawake kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Alifafanua kuwa elimu haiishii darasani pekee, bali inahusisha pia kupata maarifa kuhusu sheria, haki za binadamu na masuala mbalimbali yanayowagusa wanawake katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, aliwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na nafasi za uongozi, akisema Katiba inawapa haki ya kupiga kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki katika kufanya maamuzi ya maendeleo.
“Wanawake wanapaswa kujiamini na kujitokeza kugombea nafasi za uongozi pale wanapoona wana uwezo wa kuwatumikia wananchi. Uongozi si wa wanaume pekee,” alisisitiza.
Kwa upande wa haki za kiuchumi, Faudhia alisema wanawake wana haki ya kumiliki mali ikiwemo ardhi, nyumba na rasilimali nyingine bila ubaguzi wa kijinsia.
Aliongeza kuwa sheria za Tanzania zinatambua mchango wa mwanamke katika familia, ikiwemo kazi za nyumbani na malezi ya watoto, kama sehemu ya mchango unaoweza kuzingatiwa katika mgawanyo wa mali za ndoa.
Pia aliwataka wanawake kutambua haki zao za urithi na kutokubali kunyimwa mali za familia kutokana na mila au desturi zinazokiuka sheria.
Faudhia alisema wanawake wengi bado wanakosa haki zao kutokana na kutofahamu sheria, hivyo akawahimiza kutafuta msaada wa kisheria kutoka taasisi husika wanapokutana na changamoto zinazohusu haki zao.
Alisisitiza kuwa uelewa wa sheria na haki za msingi ni silaha muhimu kwa mwanamke katika kujenga maisha bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Ends..








Post a Comment