Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
KIONGOZI wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Gausi Salum Nyambwa, amesema maadhimisho ya Siku ya Ashura ni fursa ya kuenzi misingi ya haki, uadilifu, amani na kupinga dhulma, akisisitiza kuwa mafundisho ya Imam Hussein yanapaswa kuendelea kuwa mwongozo wa kujenga jamii yenye mshikamano.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Ashura, Nyambwa alisema siku hiyo huadhimishwa kila mwaka kwa kumbukumbu ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein, ambaye alisimama kupinga dhulma, uonevu na utawala usiozingatia haki.
Alisema lengo la maadhimisho hayo si kumbukumbu pekee, bali ni kuendeleza ujumbe wa ukweli, usawa, haki na amani katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.
"Imam Hussein alisimama kutetea haki na kupinga dhulma. Nasi tunaadhimisha siku hii kwa kuendeleza maadili hayo ili amani, umoja na mshikamano viendelee kutawala katika nchi yetu," alisema.
Nyambwa alieleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani na utulivu, hivyo aliwataka Watanzania wote kushirikiana kulinda mshikamano wa kitaifa na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko na vurugu.
Aidha, alisema Waislamu wa madhehebu ya Shia wanapinga uonevu, fujo na aina yoyote ya dhulma, huku wakiunga mkono juhudi zote zinazolenga kuimarisha maendeleo, haki na umoja nchini.
Aliongeza kuwa dini ya Kiislamu inahimiza upendo, uelewano, mshikamano na amani, na kwamba waumini wanapaswa kuishi kwa misingi ya ukweli, kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu haki za wengine.
Katika wito wake kwa Watanzania wa dini zote, Nyambwa aliwahamasisha kuendelea kuilinda Tanzania kwa kudumisha amani na mshikamano, akisema mafundisho ya Imam Hussein yanabaki kuwa alama ya kusimama upande wa haki na kupinga dhulma katika kila zama.
Alisisitiza kuwa Waislamu wataendelea kueneza maadili mema ya Uislamu pamoja na kuhamasisha amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.
ENDS..









إرسال تعليق