VIOLET AHIMIZA WANAWAKE KUNYAKUA FURSA ZA KIUCHUMI, KUJIFUNZA LUGHA ZA KIMATAIFA

 WANAWAKE WAMETAKIWA KUNYAKUA FURSA ZA KIUCHUMI, KUJIFUNZA LUGHA ZA KIMATAIFA

Na Arushadigital | ARUSHA

Wanawake wametakiwa kujitambua, kujithamini na kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazojitokeza katika maeneo yao huku wakihimizwa kuwajengea watoto wa kike uwezo wa kujifunza lugha za kimataifa ili kuendana na mahitaji ya soko la dunia.


Wito huo umetolewa na Mgeni Rasmi wa jukwaa la Khanga Gala, Violet Mfuko, wakati akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Arusha, ambapo alisisitiza kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema wanawake wamepewa uwezo mkubwa wa kusimamia familia, kulea watoto na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, hivyo wanapaswa kutumia vipaji, maarifa na fursa zilizopo ili kuboresha maisha yao na ya jamii inayowazunguka.

“Wanawake ni watu muhimu sana katika jamii. Mwanamke mwenye akili salama hujitambua, hujiheshimu na kufanya maamuzi sahihi yanayochangia maendeleo ya familia na taifa. Tunapaswa kuendelea kutumia uwezo tuliopewa kwa manufaa ya jamii yetu,” alisema Violet.

Aidha, aliwataka wanawake kuendelea kuzingatia malezi bora ya watoto na kuimarisha maadili ndani ya familia, akieleza kuwa msingi wa jamii bora huanzia nyumbani.

Katika hatua nyingine, Violet aliwahamasisha wanawake wa Arusha kujiandaa kutumia fursa zinazotarajiwa kuongezeka kutokana na ujio wa maelfu ya wageni katika mkoa huo, hususan kupitia shughuli za utalii na mikutano ya kimataifa.

Alisema ujio wa wageni hao ni nafasi muhimu kwa wanawake kujihusisha na biashara mbalimbali zitakazowaongezea kipato na kukuza uchumi wa familia zao.

“Arusha ni kitovu cha utalii na mikutano. Tunatarajia wageni wengi kuja hapa, hivyo wanawake wanapaswa kujipanga mapema na kutumia fursa hizo kwa kuanzisha au kupanua biashara zao,” alisema.

Pia aliwasihi wazazi kuwahamasisha mabinti kujifunza lugha za Kiingereza, Kifaransa na lugha nyingine za kimataifa ili kuwawezesha kuwasiliana kwa urahisi na wageni pamoja na kuongeza nafasi zao za ajira na biashara.

Alibainisha kuwa wanawake wengi tayari wameonyesha mafanikio makubwa katika sekta za biashara, huduma za hoteli na shughuli nyingine za kiuchumi, huku akieleza kuwa ujuzi wa lugha za kigeni utaongeza ushindani wao katika soko la kimataifa.

Vilevile, Violet alipongeza juhudi za kuendeleza utamaduni wa Mtanzania kupitia matumizi ya kanga, akisema mavazi hayo ni sehemu muhimu ya urithi wa taifa unaopaswa kuhifadhiwa na kuenziwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema kuendelea kuonesha na kutumia kanga zinazozalishwa nchini, ikiwemo Zanzibar, ni ishara ya jamii kuthamini tamaduni zake na kuzitumia kama nyenzo ya maendeleo na utambulisho wa taifa.

Kauli mbiu ni "Funga kanga imarisha Afya ya Akili ya Mwanamke"








Ends .

Post a Comment

أحدث أقدم