VIJANA WAHITIMU VYUO CCM WALIA AJIRA, MBUNGE SELINA AAHIDI KUENDELEA KUWATETEA

VIJANA WAHITIMU WALIA AJIRA, SELINA KINGALAME AAHIDI KUENDELEA KUWATETEA

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA 

WAHITIMU wa vyuo vikuu na vyuo vya kati mkoani Arusha wameiomba Serikali kuongeza fursa za ajira, mafunzo kwa vitendo na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri, wakieleza kuwa ukosefu wa ajira na hitaji la uzoefu wa kazi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili mara baada ya kuhitimu masomo yao.


Wito huo ulitolewa na wahitimu mbalimbali wakati wa hafla ya mahafali iliyowakutanisha vijana kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu, ambapo walieleza kuwa licha ya kupata elimu na ujuzi wa kitaaluma, wengi wao bado wanakumbana na ugumu wa kupata nafasi katika soko la ajira.


Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Said Rajabu  kutoka Wilaya ya Monduli alisema vijana wengi hukosa ajira kutokana na masharti ya waajiri wanaohitaji uzoefu wa kazi wa miaka miwili hadi mitatu, hali inayowanyima nafasi wahitimu wapya kuingia kwenye ajira rasmi.


“Tunaiomba Serikali kuweka mikakati maalum ya kuhakikisha vijana wanaohitimu vyuo wanapata ajira. Mara nyingi tunaambiwa tunahitaji uzoefu wa miaka miwili au mitatu ilhali ndiyo kwanza tumemaliza masomo,” alisema.


Said pia aliitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia wahitimu mitaji na programu za uwezeshaji wa kiuchumi ili waweze kujiajiri na kutumia elimu waliyoipata katika kujenga uchumi wao na wa taifa.


Alisema vijana wengi waliokuwa wakishiriki shughuli za uongozi na maendeleo vyuoni hujikuta wakisahaulika mara baada ya kuhitimu, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee ili kuwapa nafasi ya kuchangia maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Viti Maalum kupitia kundi la vijana, Selina Kingalame, alisema amesikia na kuelewa changamoto zinazowakabili wahitimu na kuahidi kuendelea kuwa sauti yao katika vyombo vya maamuzi.


Kingalame alisema ataendelea kusimamia masuala ya vijana bungeni kwa kushinikiza upatikanaji wa ajira, fursa za uwezeshaji wa kiuchumi na mazingira bora yatakayowawezesha kutumia elimu yao katika kujiletea maendeleo.


“Vijana ni nguvu kazi muhimu ya taifa. Nitaendelea kuwasemea na kutetea maslahi yao ili kuhakikisha changamoto wanazokabiliana nazo zinapatiwa ufumbuzi,” alisema.


Hata hivyo, aliwataka wahitimu kutokuweka matumaini yao katika ajira za kuajiriwa pekee, bali kujiongezea ujuzi, kutumia ubunifu na kuthubutu kuanzisha shughuli za kujiajiri zitakazowawezesha kujitegemea kiuchumi.


“Mbali na kusubiri ajira rasmi, vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kuangalia namna ya kujiajiri kupitia ujuzi na elimu waliyoipata. Fursa zipo na zinahitaji vijana wenye uthubutu kuzitumia,” alisema.


Mbunge huyo alibainisha kuwa suala la uzoefu wa kazi limeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wahitimu wengi wanaoingia kwa mara ya kwanza katika soko la ajira, akiahidi kuendelea kulisemea ili kutafuta suluhisho litakalowapa nafasi vijana wenye elimu na uwezo kuonyesha vipaji vyao.


Aidha, aliitaka Serikali kuendelea kupanua programu za mafunzo kwa vitendo, uwezeshaji wa vijana na uanzishaji wa miradi ya kiuchumi inayoweza kunufaisha wahitimu wanaomaliza masomo kila mwaka.


Kingalame alihitimisha kwa kuwataka vijana kutokata tamaa mbele ya changamoto za ajira, bali waendelee kujifunza, kujiongezea ujuzi na kutumia fursa zinazojitokeza ili kujenga mustakabali bora wa maisha yao.


Kauli za wahitimu hao na ahadi za mbunge huyo zimeibua matumaini mapya kwa vijana wengi wanaomaliza masomo kila mwaka, huku wakitarajia kuona hatua zaidi zikichukuliwa katika kuongeza ajira na fursa za uwezeshaji wa kiuchumi nchini.

Post a Comment

أحدث أقدم