TANZANIA YAAHIDI KUIMARISHA MIFUMO YA UTABIRI NA TAHADHARI ZA MAPEMA ZA HALI YA HEWA

 Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

TANZANIA imesema itaendelea kuimarisha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa na huduma za tahadhari za mapema ili kulinda maisha ya wananchi na kuongeza usalama na ufanisi katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan sekta ya usafirishaji, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa uchukuzi ,Prof Makame Mnyaa,Juni 29,2026 jijini Arusha wakati akifungua Warsha ya Nne ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)) kuhusu Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Matumizi ya Kiutendaji (Operational Climate Prediction – OCP-4), inayowakutanisha wataalamu wa hali ya hewa, wanasayansi na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Prof Mnyaa, alisema sekta ya uchukuzi inategemea kwa kiwango kikubwa taarifa sahihi na za wakati kuhusu hali ya hewa, akisisitiza kuwa uwekezaji katika huduma za hali ya hewa ni uwekezaji katika usalama wa wananchi na ufanisi wa uchumi wa taifa.

“Usafiri wa anga, baharini na barabarani unategemea sana taarifa sahihi za hali ya hewa. Hivyo, uwekezaji katika huduma za hali ya hewa ni uwekezaji katika usalama wa watu na ufanisi wa uchumi wetu,” alisema Profesa Mnyaa.

Alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha sayansi ya hali ya hewa, teknolojia za kisasa na miundombinu ya uchunguzi wa tabianchi ili kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakuwa salama zaidi na yenye ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema Tanzania inaendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa, akisisitiza kuwa majanga ya tabianchi hayana mipaka ya kisiasa.

“Ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni msingi muhimu katika kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Ko Barrett, amesema dunia inahitaji kuimarisha mifumo ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa na huduma za tabianchi ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati na kusaidia kuchukua hatua za mapema dhidi ya majanga.

Akizungumza katika warsha hiyo, Barrett amesema OCP-4 ni ya kihistoria kwani kwa mara ya kwanza inafanyika barani Afrika, hatua inayoonyesha kuongezeka kwa mchango wa bara hilo katika maendeleo ya huduma za hali ya hewa duniani.

Ameipongeza Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa (Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)) kwa maandalizi mazuri na uongozi wake katika kuandaa mkutano huo muhimu.

Barrett alisema tangu kuanzishwa kwa mfululizo wa warsha hizo mwaka 2015, kumekuwa na mafanikio katika kuunganisha utafiti wa kisayansi na matumizi ya kiutendaji, lakini bado kuna haja ya kuhakikisha taarifa za kisayansi zinatafsiriwa kuwa huduma zinazosaidia maamuzi ya moja kwa moja kwa jamii.

Alieleza kuwa mifumo kama Climate Services Information System (CSIS) pamoja na WMO Integrated Processing and Prediction System (WIPPS) ni nguzo muhimu zinazowezesha utabiri wa matukio ya tabianchi, ikiwemo El Niño, na kusaidia nchi kupanga mapema.

Aidha, Barrett amesisitiza umuhimu wa mpango wa “Early Warnings for All” unaotekelezwa na Umoja wa Mataifa, akisema ni muhimu hasa barani Afrika katika kuokoa maisha dhidi ya majanga ya asili.

Katika hotuba yake, ameongeza kuwa teknolojia ya akili mnemba (AI) inaleta mapinduzi makubwa katika utabiri wa hali ya hewa kwa kuongeza kasi na usahihi wa taarifa, lakini akisisitiza haitakiwi kuchukua nafasi ya wataalamu wa kitaifa bali kuwa nyenzo ya kuwaimarisha.

Barrett alihitimisha kwa kuahidi kuwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) itaendelea kushirikiana na nchi wanachama na wadau wa maendeleo kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa ajili ya maendeleo endelevu na usalama wa binadamu.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema matokeo ya OCP-4 yatatumika kuboresha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika maamuzi ya maendeleo.

Alisema warsha hiyo imewakutanisha wataalamu kujadili mnyororo mzima wa huduma za hali ya hewa kuanzia uzalishaji wa utabiri hadi namna unavyoweza kubadilishwa kuwa huduma zinazosaidia maamuzi ya kiuchumi na kijamii.

Alishukuru washirika wa maendeleo akiwemo Ubalozi wa Ireland, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), NORAD na wadau wengine kwa mchango wao.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeji, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema ni heshima kubwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, akibainisha kuwa Arusha imeendelea kuwa kitovu cha mikutano na diplomasia ya kimataifa.

Alisema wageni wa warsha hiyo wanatarajiwa pia kutembelea vivutio vya utalii kama Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Ziwa Manyara, Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru, akisisitiza kuwa mazingira ya Arusha na Kilimanjaro yana mchango mkubwa katika mifumo ya tabianchi ya kikanda na kimataifa.

Warsha hiyo imewakutanisha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kujadili namna bora ya kuimarisha huduma za utabiri wa hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema ili kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi duniani.








Ends .

Post a Comment

أحدث أقدم