SIMBU, ZARA TOURS WAITUMIA KARIBU-KILIFAIR KUITANGAZA TANZANIA DUNIANI,SIMBU AZINDUA “KIMBIA NA SIMBU”, AHAMASISHA UTALII WA MICHEZO

SIMBU, ZARA TOURS WAITUMIA KARIBU-KILIFAIR KUITANGAZA TANZANIA DUNIANI,SIMBU AZINDUA “KIMBIA NA SIMBU”, AHAMASISHA UTALII WA MICHEZO

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

NYOTA wa mbio ndefu Tanzania, Alphonce Simbu, ameungana na kampuni ya Zara Tanzania Adventures kuhamasisha utalii na michezo kama nyenzo muhimu za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia Maonesho ya Karibu-Kilifair yanayoendelea jijini Arusha.


Simbu alikuwa miongoni mwa mamia ya washiriki wa mashindano ya Summit Run Challenge, yanayodhaminiwa na Zara Tours kwa lengo la kuhamasisha utalii wa michezo na kuutangaza Mlima Kilimanjaro pamoja na vivutio vingine vya Tanzania kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali.

 

Akizungumza katika tukio hilo, Simbu alisema michezo na utalii vina uhusiano mkubwa katika kuitangaza Tanzania duniani, akibainisha kuwa mafanikio ya wanamichezo wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa huchochea watu wengi kutaka kufahamu zaidi kuhusu nchi, hifadhi zake na vivutio vyake vya utalii.


“Michezo husafirisha ujumbe kwa haraka duniani. Michezo na utalii vinapounganishwa vinakuwa nguvu kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa,” alisema Simbu huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro kama kivutio kikubwa cha utalii barani Afrika.


Katika hafla hiyo, Simbu pia alitambulisha rasmi kampeni ya “Kimbia na Simbu”, inayolenga kuwaunganisha Watanzania katika safari yake ya maandalizi kuelekea mashindano ya Sydney Marathon 2026 nchini Australia, sambamba na kusaidia kukuza vipaji vya wanariadha chipukizi nchini.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Zara Tanzania Adventures, Nancy Ngotea, alisema Karibu-Kilifair imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kufungua masoko mapya ya utalii, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa.


Alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuendeleza utalii na michezo, akisisitiza kuwa sekta hizo mbili zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, afya za wananchi na kuijengea Tanzania taswira chanya duniani.


Nancy aliwapongeza wanariadha wanaoiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kuwataka kutumia michezo kama fursa ya kujifunza, kukuza vipaji na kuwa mabalozi wazuri wa taifa.


Mashindano ya Summit Run Challenge yamekuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya Karibu-Kilifair mwaka huu, huku washiriki wakishindania zawadi za fedha taslimu zenye thamani ya hadi shilingi milioni moja na kubeba ujumbe wa kuunganisha michezo, utalii na maendeleo ya taifa.




Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم