MAZISHI YAGEUKA UWANJA WA MGOGORO SIHA, JENEZA LAWEKWA JUU YA GARI LA DC


MAZISHI YAGEUKA UWANJA WA MGOGORO SIHA, JENEZA LAWEKWA JUU YA GARI LA DC

Na Arushadigital | Siha, Kilimanjaro

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, jeneza lenye mwili wa aliyekuwa dereva wa bodaboda, Emmanuel Mwanry, liliwekwa juu ya gari la Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk. Christopher Timbuka, na kundi la vijana wenye hasira, hali iliyosababisha mazishi kusimama kwa saa kadhaa huku mamia ya waombolezaji wakibaki katika sintofahamu.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Ngirinyi, Kata ya Levishi, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, ambapo kilichotarajiwa kuwa siku ya mwisho ya kumuaga marehemu kiligeuka kuwa uwanja wa mvutano mkali kati ya wananchi na mamlaka.

Waombolezaji waliokuwa wamekusanyika tangu mchana kwa ajili ya mazishi walijikuta wakisubiri kwa muda mrefu baada ya kundi la vijana kusisitiza kuwa shughuli za maziko haziwezi kuendelea hadi wenzao 10 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi waachiwe huru.

Kadiri muda ulivyokuwa ukisonga, hali ya maombolezo ilibadilika na kuwa ya taharuki na hasira. Vijana hao walichukua hatua ya kuliondoa jeneza eneo la mazishi na kuliweka juu ya gari la Mkuu wa Wilaya kama ishara ya kupinga kile walichodai kuwa ni kutotendewa haki.

Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi na waombolezaji waliokuwa wamefika kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, huku shughuli zote za mazishi zikisitishwa kusubiri suluhu ya mgogoro huo.

Baadhi ya waombolezaji waliokuwa wamekaa eneo hilo kwa zaidi ya saa sita walionekana kuchoshwa na hali hiyo na kuanza kuondoka baada ya kutokuwepo kwa mwafaka kuhusu hatima ya mazishi hayo.

Akizungumza mbele ya wananchi waliokuwa eneo la tukio, mmoja wa vijana hao, Nickson Nkya, alisema hawakuwa tayari kuona mwili wa marehemu ukizikwa huku wenzao wakiendelea kushikiliwa na polisi.

“Hatuwezi kumzika mwenzetu mpaka wenzetu waliokamatwa waachiwe. Pia tunataka pikipiki ya marehemu irejeshwe. Tunaamini haki bado haijatendeka na hatuwezi kukubali kuendelea kuonewa,” alisema Nkya.

Licha ya juhudi za viongozi wa eneo hilo, ndugu wa marehemu na wazee wa kijiji kutafuta muafaka, vijana hao waliendelea kushikilia msimamo wao wakitaka madai yao yashughulikiwe kwanza kabla ya mazishi kuendelea.

Hadi jioni ya siku hiyo, hali ilikuwa bado ya sintofahamu huku mwili wa marehemu ukiwa haujazikwa na mamia ya wananchi wakiendelea kusubiri hatua za mamlaka husika ili kumaliza mvutano huo.

Tukio hilo limeacha maswali mengi katika jamii kuhusu athari za migogoro kati ya wananchi na vyombo vya dola, hasa pale inapogusa shughuli nyeti za kijamii kama mazishi, huku familia ya marehemu ikibaki katika majonzi makubwa ikisubiri kumpumzisha mpendwa wao katika safari yake ya mwisho.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post