WAWEKEZAJI WAZAWA WAPONGEZA TANZANIA INVESTMENT SUMMIT KWA KUWAFUNGULIA FURSA ZA MITAJI
Na Joseph Ngilisho | Arusha
WAWEKEZAJI wazawa wamepongeza Mkutano wa Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Summit) kwa kueleza kuwa umekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha na taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo, hatua inayochochea upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika jijini Arusha, mwakilishi wa kampuni ya Wazawa Green Energy Limited, Eric Mora Magige, alisema mkutano huo umefungua fursa mpya kwa wawekezaji wa ndani kukutana ana kwa ana na taasisi za fedha za ndani na kimataifa zenye uwezo wa kufadhili miradi ya maendeleo.
Magige alisema kampuni yao kwa sasa inatekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme kupitia nishati ya biomasi (Biomass Energy) mkoani Rukwa, katika eneo la Sumbawanga, na kwamba kupitia mkutano huo wamefanikiwa kufanya mazungumzo ya awali na wadau mbalimbali wa kifedha wanaoweza kusaidia upatikanaji wa mtaji wa kuendeleza mradi huo.
“Tumepata nafasi ya kukutana na taasisi mbalimbali za kifedha na wawekezaji wenye uwezo wa kuingia ubia nasi. Hii ni fursa kubwa kwa kampuni za wazawa ambazo mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi mikubwa,” alisema Magige.
Alieleza kuwa mradi wa uzalishaji wa umeme kupitia biomasi una lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati safi na endelevu nchini, huku ukiwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini kupitia matumizi ya malighafi zinazopatikana ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa Magige, Tanzania Investment Summit imekuwa daraja muhimu linalowawezesha wawekezaji kuwasilisha miradi yao kwa taasisi za fedha, mifuko ya uwekezaji na washirika wa maendeleo, jambo linaloongeza uwezekano wa miradi hiyo kufikia hatua ya utekelezaji kwa haraka zaidi.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hali inayowavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za kifedha ni msingi muhimu wa kufanikisha ajenda ya maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa mikutano kama hiyo inapaswa kuendelea kufanyika mara kwa mara ili kuwapa wawekezaji wa ndani nafasi kubwa zaidi ya kupata mitaji na masoko ya miradi yao.
Mkutano wa Uwekezaji Tanzania umezikutanisha taasisi za fedha, wawekezaji, viongozi wa Serikali na washirika wa maendeleo kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa mitaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Ends


إرسال تعليق