LULU MWACHA: VIJANA WAENDELEE KUIAMINI CCM NA KUTUMIA FURSA ZA MAENDELEO, AFCON NI FURSA KUBWA YA KIUCHUMI

LULU MWACHA: VIJANA WAENDELEE KUIAMINI CCM NA KUTUMIA FURSA ZA MAENDELEO, AFCON NI FURSA KUBWA YA KIUCHUMI

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU 

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Vijana, Lulu Mwacha, amewataka vijana nchini kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kujiletea maendeleo na kuchangia ukuaji wa taifa.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika eneo la Ngaramtoni, wilayani Arumeru, mkoani Arusha, wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenan Kihongosi, Mwacha aliwashukuru wananchi kwa kuendelea kukiamini chama hicho na viongozi wake katika ngazi mbalimbali.


Alisema mafanikio makubwa ya maendeleo yanayoonekana nchini ni matokeo ya uongozi thabiti wa CCM chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuwatumikia wananchi kwa upendo na kujali mahitaji yao.


“Tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi, kumchagua Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa CCM. Niwaombe muendelee kukiamini chama hiki kwa sababu ndicho kinachoendelea kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta mbalimbali,” alisema Mwacha.


Mbunge huyo alieleza kuwa serikali ya CCM imeendelea kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha mazingira ya uwekezaji, ajira na ujasiriamali, hatua ambazo zimefungua fursa nyingi kwa vijana nchini.


Aidha, alizitaka mamlaka husika kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu inawafikia walengwa kwa wakati ili kuwawezesha kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.


Mwacha pia aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali katika sekta mbalimbali, akisema vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na msingi wa maendeleo ya baadaye.


“Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele kutumia fursa zilizopo katika elimu, ujasiriamali, kilimo, mifugo na teknolojia ili kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” alisema.


Katika hotuba yake, Mwacha aliwahamasisha vijana kuanza kujiandaa kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.


Alisema mashindano hayo yatafungua fursa nyingi za biashara, ajira na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, usafirishaji, huduma za malazi, migahawa, biashara za bidhaa za kumbukumbu pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazolenga kuhudumia wageni na watalii watakaotembelea nchi hizo.


“Tunapoelekea AFCON 2027, vijana tusisubiri kuajiriwa pekee. Tunapaswa kuwa wabunifu, kubuni biashara na kujiandaa kutumia fursa zitakazotokana na mashindano hayo makubwa. Hii ni nafasi ya kipekee ya kubadilisha maisha ya vijana wengi kiuchumi,” alisema.


Aliongeza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miundombinu na kuboresha mazingira ya biashara ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa wanufaika wakuu wa fursa zitakazotokana na mashindano hayo ya kimataifa.


Mbunge huyo alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi na kufanya maamuzi yanayolenga kuboresha ustawi wa wananchi.


Alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Arumeru kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano katika kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na CCM na serikali yake.


“Tuendelee kushikamana, tukiamini chama chetu na viongozi wetu ili maendeleo yaendelee kuwafikia wananchi wote. Kidumu Chama Cha Mapinduzi, kidumu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Ends 

Post a Comment

أحدث أقدم