JIJI LA ARUSHA LATENGA BILIONI 3.27 KUBORESHA BARABARA NA MIFEREJI YA MAJI YA MVUA

 JIJI LA ARUSHA LATENGA BILIONI 3.27 KUBORESHA BARABARA NA MIFEREJI YA MAJI YA MVUA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 



MEYA wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, amesema halmashauri hiyo imeanza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara, mifereji ya maji ya mvua na makalavati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani zinazotokana na kodi zinazolipwa na wananchi.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Arusha leo, Iranghe alisema Baraza la Madiwani katika bajeti ya mwaka wa fedha uliopita lilitenga shilingi bilioni 3.272 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jiji, hususan yale yanayokabiliwa na changamoto za usafiri kutokana na uharibifu wa barabara na athari za mvua.


Alisema ni muhimu wananchi kufahamu kuwa kodi wanazolipa ndizo zinazorejeshwa kwao kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha yao.


"Kodi zinazolipwa na wananchi ndizo zinazorejeshwa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo. Tunataka wananchi wajue fedha zao zinatumika wapi na kwa manufaa gani," alisema Iranghe.


Meya huyo alieleza kuwa tayari mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo imesainiwa na wakandarasi wameanza maandalizi ya kuingia katika maeneo ya kazi. Alibainisha kuwa kipaumbele kikubwa kimetolewa katika ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, makalavati madogo na makubwa (box culverts) ili kudhibiti mafuriko na kulinda miundombinu ya barabara.


Kwa mujibu wa Iranghe, kampuni ya Razz Builders Limited imepewa zabuni ya kujenga box culvert pamoja na mifereji ya maji ya mvua katika eneo la Kiboko Juu–Majimbo hadi Bumiko, lililopo Kata ya Olasiti.


Aidha, kampuni ya Mandaka Tanzania Limited inatekeleza mradi wa ujenzi wa box culvert na mifereji ya maji ya mvua katika barabara za Banana, Hazina, Safina na Kitwekijwa zilizopo katika kata za Baraa na Kimandolu. Mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi milioni 585.


Katika mradi mwingine mkubwa, kampuni ya Mjiangziyo Engineering Group Corporation Limited inajenga Barabara ya Liwili kwa kiwango cha zege yenye urefu wa zaidi ya kilomita moja kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 1.8.


Iranghe alisema matumizi ya teknolojia ya zege katika baadhi ya barabara ni mkakati wa kuongeza uimara wa miundombinu na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara zinazojitokeza katika baadhi ya barabara za lami.


Alifafanua kuwa kwa ujumla miradi yote inayotekelezwa chini ya mpango huo inatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.7, huku ikilenga kuondoa changamoto za usafiri na mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji.


Meya huyo aliwataka wananchi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwa fedha zinazotumika ni mali yao kupitia kodi wanazolipa, hivyo wana haki ya kujua maendeleo na thamani ya fedha zinazowekezwa.


Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai hakuna maendeleo yanayoendelea katika jiji hilo kutokana na kutofahamu miradi inayotekelezwa katika kata nyingine tofauti na wanazoishi.


"Si kila kata imefikiwa kwa wakati mmoja. Leo miradi inaweza kutekelezwa Terati, Olasiti au Kimandolu, lakini wananchi wa kata nyingine wasione kana kwamba hakuna kinachoendelea. Rome haikujengwa kwa siku moja," alisema.


Iranghe aliongeza kuwa katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai mwaka huu, zaidi ya shilingi bilioni saba zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kuboresha barabara, madaraja, vivuko na mifereji ya maji ya mvua katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.


Alisisitiza kuwa lengo la Jiji la Arusha ni kuhakikisha barabara za vumbi zinaboreshwa kwa kiwango kinachostahili sambamba na kujenga mifumo imara ya kupitisha maji ya mvua ili kupunguza uharibifu wa miundombinu na kuongeza usalama wa wananchi.

"Mamlaka ya Jiji la Arusha inaendelea kufanya kazi na matokeo yanaonekana.


 "Tunawaomba wananchi waendelee kuiunga mkono serikali na halmashauri yao kwa kulipa kodi, kwani fedha hizo ndizo zinazorejea kwao kupitia miradi ya maendeleo," alisisitiza.


ENDS...

Post a Comment

أحدث أقدم