ESCAPE LODGE SERENGETI YAJA NA DIRA MPYA YA UTALII WA KIFAHARI KATIKATI YA HIFADHI YA SERENGETI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAKATI Tanzania ikiendelea kuimarisha nafasi yake kama moja ya vinara wa utalii barani Afrika, kampuni ya Escape Lodge Serengeti imejitokeza na uwekezaji mpya unaolenga kubadilisha uzoefu wa watalii kwa kuwapatia huduma za kifahari zinazounganisha anasa za kisasa na mazingira halisi ya asili ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Rays alisema Escape Lodge Serengeti ipo katika eneo la Serengeti Central, Nyabogati Gate 8 (Bogati), umbali wa takribani kilomita 30 kutoka uwanja wa ndege, na imejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya huduma za malazi ya kifahari.
“Dhamira yetu ni kuwapa wageni zaidi ya sehemu ya kulala. Tunataka wapate nafasi ya kuishi na kuhisi uzuri wa Serengeti huku wakifurahia huduma bora za kiwango cha juu katika mazingira salama na yenye faragha,” alisema Rays.
Kwa mujibu wa Rays, nyumba za familia zimewekewa maeneo maalum ya kukaa pamoja na kufurahia muda wa kifamilia huku zikitoa mwonekano mpana wa mazingira ya porini, wakati vyumba vya wageni binafsi vinatoa faragha kamili kwa wanaotafuta utulivu na mapumziko ya kipekee.
Aliongeza kuwa vyumba vyote vina milango mikubwa inayowezesha wageni kufurahia mandhari ya Serengeti moja kwa moja, huku vikijumuisha huduma za kisasa kama mabafu ya ndani, beseni za kuogea na mabafu ya nje yaliyojengwa kwa kutumia malighafi za asili ili kuongeza mguso wa mazingira ya porini.
Mbali na huduma za malazi, Rays alisema Escape Lodge Serengeti imewekeza katika miundombinu rafiki kwa familia kwa kuwa na mgahawa wa kisasa, eneo la watoto kucheza pamoja na maktaba yenye vitabu vinavyoelezea historia, urithi na wanyamapori wa Serengeti.
“Tunataka wageni wetu waondoke hapa wakiwa si tu wamepumzika, bali pia wamejifunza kuhusu urithi wa Serengeti na umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za asili,” alisema.
Aidha, alisema uwekezaji huo ni wa kwanza kwa kampuni hiyo nchini Tanzania na umeanzia Serengeti kutokana na hadhi yake ya kimataifa kama moja ya vivutio vikubwa vya utalii duniani.
“Serengeti ni chapa inayotambulika duniani kote. Kuanzisha uwekezaji wetu hapa ni sehemu ya mkakati wa kuitangaza Tanzania na kuonyesha uwezo mkubwa uliopo katika sekta ya utalii,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Escape Lodge Serengeti, Job Constantine, alisema Lodge hiyo itaendelea kuimarisha huduma zake kwa lengo la kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotafuta malazi ya kifahari yenye utofauti wa kipekee.
Constantine alisema moja ya sifa kubwa za lodge hiyo ni eneo ilipojengwa, ambalo liko katika mwinuko unaowawezesha wageni kufurahia mandhari pana ya Serengeti na kushuhudia wanyamapori mbalimbali wakiwa katika mazingira yao ya asili.
“Tunajivunia kuwa sehemu ya wadau wanaochangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Wageni wanaofika kwetu hupata mchanganyiko wa huduma bora, ukarimu wa hali ya juu na uzoefu wa kipekee wa kuiona Serengeti kwa ukaribu zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa ushiriki wa Escape Lodge Serengeti katika maonesho ya KARIBU-KILIFAIR ni sehemu ya mkakati wa kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii Afrika, huku ukitoa fursa ya kukutana na mawakala wa safari, wawekezaji na watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Constantine aliwataka watalii wanaopanga kutembelea Serengeti kufika katika lodge hiyo ili kujionea huduma zake za kifahari na mazingira ya kipekee yanayoifanya kuwa moja ya vivutio vipya katika sekta ya malazi ya utalii nchini.
Maonesho ya KARIBU-KILIFAIR yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka Tanzania na nje ya nchi kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii, huduma za malazi pamoja na fursa za uwekezaji zinazochochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta hiyo muhimu.
***Ends***




إرسال تعليق