DKT. LUKUMAY AIOMBA CCM KUSAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA BARABARA, MAJI NA ARDHI ARUMERU MAGHARIBI
Na Joseph Ngilisho | Ngaramtoni, Arumeru
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameiomba Serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuharakisha utatuzi wa changamoto za barabara, maji na migogoro ya ardhi zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Dkt. Lukumay alitoa ombi hilo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Ngaramtoni mkoani Arusha, ulioongozwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Taifa, Kenan Kihongosi ambaye yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza kero za wananchi.
Katika hotuba yake, Dkt. Lukumay alisema wananchi wa Arumeru Magharibi bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali, akitaja barabara za Sokoni–Bangata, Lunguya Seliani–Mlinga, Chiprai–Likamba, Kilimamoto–Mandete pamoja na Sambasha Mjini–Motoni hadi Ngaramtoni kuwa zinahitaji maboresho ya haraka.
Alieleza kuwa ubovu wa barabara hizo umekuwa ukikwamisha usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na shughuli za biashara, hivyo kuathiri maisha ya wananchi.
Mbunge huyo pia aliomba kuharakishwa kwa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 18 kutoka Mianzini hadi Ngaramtoni, akisema mradi huo utakuwa kichocheo muhimu cha maendeleo katika eneo hilo.
“Kuna wananchi ambao bado wanashindwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutokana na hali mbaya ya barabara. Tunaiomba Serikali na chama chetu kuendelea kutusaidia ili maeneo haya yaweze kufunguliwa zaidi kiuchumi,” alisema Dkt. Lukumay.
Katika sekta ya maji, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maji, lakini akaomba fedha zilizobaki katika baadhi ya miradi zitolewe kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma stahiki.
Alitaja mradi wa maji wa Ngosambu kuwa miongoni mwa miradi inayohitaji fedha za nyongeza ili kukamilika, akieleza kuwa wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya maji yenye kiwango kikubwa cha fluoride ambacho kinaathiri afya zao.
Aidha, alieleza kuwa kukamilika kwa miradi ya maji katika maeneo ya Ulimbu, Nyamula, Laroi na Wanjoro kutasaidia kuondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama.
Mbali na hilo, Dkt. Lukumay aliibua suala la migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, akisema wananchi wamekuwa wakihitaji ufumbuzi wa kudumu ili waweze kuendelea na shughuli zao za maendeleo bila hofu.
Alisema viongozi wa wilaya na mkoa wamekuwa wakifuatilia masuala hayo, lakini bado kunahitajika msaada wa Serikali Kuu ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote.
Akihitimisha hotuba yake, mbunge huyo alimshukuru Katibu wa Uenezi wa CCM kwa kutembelea Arumeru Magharibi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja.
“Ziara hizi zinaonyesha namna chama na Serikali vinavyowajali wananchi. Tuna imani kwamba hoja na changamoto zilizowasilishwa leo zitapatiwa ufumbuzi kwa manufaa ya wananchi wa Arumeru Magharibi,” alisema Dkt. Lukumay.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa CCM, Serikali na mamia ya wananchi wa Ngaramtoni waliojitokeza kusikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa maoni yao kuhusu changamoto zinazowakabili.






إرسال تعليق