DKT. LUKUMAY AIBANA SERIKALI KUONGEZA BAJETI YA TARURA ARUMERU MAGHARIBI,ASEMA CHANGAMOTO YA BARABARA BADO NI KUBWA

 DKT. LUKUMAY AIOMBA SERIKALI KUONGEZA BAJETI YA TARURA ARUMERU MAGHARIBI

Joseph Ngilisho|Arushadigital, DODOMA

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika jimbo hilo kutoka Sh bilioni 2.3 za sasa hadi angalau Sh bilioni 6 ili kuboresha barabara zenye changamoto kubwa ambazo zimekuwa kero kwa wananchi na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.


Dkt. Lukumay alitoa ombi hilo bungeni leo June 8,2026 wakati akiuliza swali la nyongeza kuhusu mipango ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara katika Arumeru Magharibi, akieleza kuwa hali ya baadhi ya barabara katika jimbo hilo bado ni mbaya licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali.


Mbunge huyo alianza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA kutoka takribani Sh bilioni 944 hadi zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika mwaka wa fedha wa sasa

.

Alisema kutokana na hali ya kijiografia ya Arumeru Magharibi, eneo hilo linahitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika miundombinu ya barabara ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri na usafirishaji mwaka mzima.


Dkt. Lukumay alitaja baadhi ya barabara zinazohitaji maboresho ya haraka kuwa ni barabara za Malaluwa, Mlangarini–Bwawani, Olgilai, Sokon II–Bangata, TPRI–Lekamba, Mbauda–Loksuto pamoja na Kimamoto–Mwandeti, akisisitiza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika jimbo hilo.


“Je, Serikali iko tayari kuongeza bajeti ya TARURA katika Arumeru Magharibi kutoka Sh bilioni 2.3 za sasa hadi angalau Sh bilioni 6 ili kutatua changamoto za barabara zinazowakabili wananchi wetu?” alihoji mbunge huyo.


Akijibu swali hilo, Waziri mwenye dhamana ya TARURA alisema Serikali inatambua changamoto za kipekee za Arumeru Magharibi, hususan kutokana na mazingira yake ya volkeno ambayo husababisha gharama kubwa za ujenzi wa barabara zinazodumu kwa muda mrefu.


Waziri huyo alimpongeza Dkt. Lukumay kwa kuendelea kuwasemea wananchi wake na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya TARURA kila mwaka ili kuboresha mtandao wa barabara nchini.


Alisema Serikali kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kupitia aina za ujenzi wa barabara zinazozingatia hali za kijiografia za maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Arumeru Magharibi, ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inadumu na kuleta matokeo ya muda mrefu.


“Tunafahamu changamoto za Arumeru Magharibi na umuhimu wa kuwa na barabara imara. Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika eneo hili ili kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora inayokidhi mahitaji yao,” alisema Waziri.


Kauli hiyo imeongeza matumaini kwa wananchi wa Arumeru Magharibi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba kuboreshwa kwa mtandao wa barabara ili kurahisisha usafiri, usafirishaji wa mazao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم