DCEA ARUSHA YAIMARISHA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA 413 WAKAMATWA DC ASEMA MAPAMBANO BADO MAKUBWA

DCEA ARUSHA YAIMARISHA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA 413 WAKAMATWA DC ASEMA MAPAMBANO BADO MAKUBWA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya mkoani humo yameendelea kuzaa matunda baada ya watuhumiwa 413 kukamatwa katika operesheni mbalimbali zilizofanywa na DCEA ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Mkude ameyasema hayo leo  Juni 26,2026 jijini Arusha wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), chini ya kaulimbiu isemayo “Ubunifu wa Kimkakati: Suluhisho la Changamoto za Dawa za Kulevya.”

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya, wakiwemo viongozi wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za elimu, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia, wataalamu wa afya pamoja na makundi ya vijana, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kupambana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkude alisema maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari kwa pamoja athari za dawa za kulevya na kuimarisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeendelea kuhatarisha amani, afya na maendeleo ya jamii.

“Dawa za kulevya ni adui wa amani yetu, adui wa familia zetu na adui wa mustakabali wa watoto wetu. Tatizo hili si la mbali tena, limefika katika jamii zetu na linawaathiri vijana wa rika mbalimbali,” alisema Mkude.

Akitoa takwimu za mafanikio ya operesheni zilizotekelezwa kati ya Julai 2025 na Juni 2026, alisema jumla ya watuhumiwa 413 walikamatwa, wakiwemo wanaume 338 na wanawake 75.

Aidha, alisema kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kilikamatwa, ikiwemo kilo 1,458.26 za mirungi na kilo 2,977.03 za bangi.

“Takwimu hizi si namba za kawaida. Kila kilo iliyokamatwa ina maana ya vijana wengi kuokolewa dhidi ya uraibu, familia nyingi kuendelea kuwa salama na jamii yetu kuepushwa na madhara makubwa ya dawa za kulevya,” alisema.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na DCEA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wanaoendelea kutoa taarifa zinazowasaidia kubaini na kuwakamata wahalifu.

Hata hivyo, Mkude alionya kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, vita dhidi ya dawa za kulevya bado vinaendelea kutokana na Arusha kuwa kitovu muhimu cha biashara, utalii na mikutano ya kimataifa, hali inayoweza kuvutia mitandao ya biashara haramu ya dawa hizo.

Alisisitiza kuwa mapambano hayo hayawezi kuachiwa taasisi za serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi, wazazi, viongozi wa dini, taasisi za elimu na viongozi wa jamii.

“Tunapaswa kuwekeza zaidi katika kinga kuliko kusubiri madhara yatokee. Elimu kwa vijana, malezi bora na uimarishaji wa maadili ni silaha muhimu katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.

Mkude pia alipongeza juhudi za DCEA katika utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali yakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo, waendesha bodaboda, wachimba madini, wasanii, wazazi na viongozi wa jamii.

Alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za matibabu, ushauri nasaha na urekebishaji wa waathirika wa dawa za kulevya zinaimarishwa kupitia vituo maalumu vya tiba na nyumba za uangalizi wa waraibu waliopona (sober houses).

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu na maeneo yanayotumika katika biashara ya dawa za kulevya ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya janga hilo.

Kwa upande wao, wadau walioshiriki maadhimisho hayo walisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, jamii na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya vinakuwa endelevu na vyenye mafanikio makubwa zaidi.

Ends .

Post a Comment

Previous Post Next Post