BALOZI MATINYI AWAHIMIZA WAFANYABIASHARA TANZANIA KUSHIRIKI MAONESHO MAKUBWA YA KIMATAIFA ALGIERS

BALOZI MATINYI AWAHIMIZA WAFANYABIASHARA TANZANIA KUSHIRIKI MAONESHO MAKUBWA YA KIMATAIFA ALGIERS

Na Arusha Digital | Algiers

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, ametoa wito kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali nchini Tanzania kutumia fursa ya kushiriki katika Maonesho ya 57 ya Kimataifa ya Biashara ya Algiers (FIA) yatakayofanyika kuanzia Juni 22 hadi 27, 2026, jijini Algiers nchini Algeria.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa miongoni mwa makubwa zaidi barani Afrika na yatahusisha kampuni zaidi ya 700 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani, yakitoa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa.

Balozi Matinyi alitoa wito huo baada ya kutembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika yaliyofunguliwa Juni 6, 2026, jijini Algiers na Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa Algeria, Kamel Rezig. Maonesho hayo yamewakutanisha washiriki kutoka Algeria pamoja na nchi 27 za Afrika.

Akizungumzia maandalizi ya maonesho yajayo, Balozi Matinyi alisema kuwa maonesho hayo yanaandaliwa na Kampuni ya Maonesho na Biashara ya Nje ya Algeria (SAFEX) na yatatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupata masoko mapya, kuanzisha ubia wa kibiashara, kubadilishana uzoefu na maarifa, pamoja na kusaini mikataba ya biashara na uwekezaji.

Alibainisha kuwa sekta zitakazonufaika zaidi ni pamoja na kilimo na ufugaji, viwanda, madini, nishati, usafirishaji, ujenzi, utalii, huduma za kifedha na teknolojia.

Katika maonesho ya Afrika yanayoendelea kwa sasa, kampuni ya Jordan ya Riad Hanieh Food Supplies, yenye tawi nchini Tanzania, imekuwa miongoni mwa washiriki waliovutia wageni wengi kwa kuonesha bidhaa zinazotokana na mazao ya Tanzania pekee, ikiwemo kahawa, korosho, karafuu, vanila na viungo mbalimbali vinavyouzwa katika masoko ya kimataifa.

Wakati huo huo, jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Algeria zimepata msukumo mpya baada ya Balozi Matinyi kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni ya GETEX inayomilikiwa na Serikali ya Algeria.

Mazungumzo hayo yalizaa makubaliano ya awali ya kampuni hiyo kutembelea Tanzania kwa lengo la kutafuta malighafi ya ngozi na kuchunguza uwezekano wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata ngozi nchini kwa ajili ya kuhudumia viwanda vyake vilivyopo Algeria.

“Tutakwenda Tanzania kutafuta ngozi na kuangalia uwezekano wa kufungua kiwanda cha kuchakata ngozi huko Tanzania kwa ajili ya viwanda vyetu hapa Algeria,” alisema Abdelkader Hamdi Mansour.

Katika mazungumzo hayo pia alikuwepo Ghersa Yahia.

Balozi Matinyi amesema wafanyabiashara na wadau wote wa Tanzania wanaotaka kushiriki au kutembelea maonesho hayo wanaweza kupata taarifa zaidi kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria, Ubalozi wa Algeria nchini Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo Biashara Tanzania (TanTrade) au Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo utasaidia kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Afrika Kaskazini na Ulaya, huku ukifungua milango mipya ya uwekezaji na ajira kupitia ushirikiano wa kibiashara unaoendelea kuimarika kati ya Tanzania na Algeria.


 


Post a Comment

Previous Post Next Post