WALIOFUNGUA KESI YA MGAWANYO WA MALI CHADEMA WAANGUKIA PUA ,MAHAKAMA KUU YAIFUTILIA MBALI

MAHAKAMA KUU YAFUTA KESI YA MGAWANYO WA RASILIMALI CHADEMA

By Arushadigital | Dar es Salaam

Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imeifuta kesi ya madai iliyokuwa ikihusu mgawanyo usio sawa wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilikuwa imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikaji hao walikuwa wakidai kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria na kutokuwepo kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali za chama hicho kati ya upande wa Bara na Zanzibar.

Akitoa uamuzi wa kesi hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, David Ngunyale alisema hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani ilikuwa na kasoro za kisheria zilizofanya kesi hiyo kushindwa kuendelea kusikilizwa.

Jaji Ngunyale alieleza kuwa walalamikaji walishindwa kubainisha kwa uwazi ni lini mgogoro huo wa madai kuhusu mgawanyo wa rasilimali ulianza, jambo ambalo ni msingi muhimu katika usikilizwaji wa kesi za madai mahakamani.

Kutokana na upungufu huo wa kisheria, Mahakama ikaona kuwa hati ya madai haikukidhi matakwa ya sheria na hivyo kuamuru kesi hiyo kufutwa.

Uamuzi huo unakuja katika kipindi ambacho vyama vya siasa nchini vinaendelea kujadili masuala ya uwakilishi, usawa wa rasilimali na uimarishaji wa mifumo ya kiutawala ndani ya taasisi zao.

Ends

Post a Comment

0 Comments