JKT YAWATAKA WAHITIMU WA KIDATO CHA SITA 2026 KURIPOTI MAKAMBINI JUNI
Na Dorine Aloyce | DODOMA
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana wote waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026 kutoka shule za Tanzania Bara na Zanzibar kuripoti katika makambi mbalimbali ya jeshi hilo kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya lazima kwa mujibu wa sheria.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Mkuu wa JKT Tawi la Utawala, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele.
Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana hao wanapaswa kuripoti katika makambi waliopangiwa kuanzia Juni 1 hadi Juni 7, 2026, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kuitikia wito huo wa taifa kwa ajili ya kujengewa uzalendo, nidhamu, uwajibikaji pamoja na stadi mbalimbali za maisha.
Amesema JKT limeandaa makambi mbalimbali nchini kwa ajili ya kupokea wahitimu hao, yakiwemo Rwamkoma JKT mkoani Mara, Msange JKT mkoani Tabora, Ruvu JKT na Kibiti JKT mkoani Pwani, pamoja na Mpwapwa JKT na Makutupora JKT mkoani Dodoma.
Makambi mengine ni Mafinga JKT mkoani Iringa, Mlale JKT mkoani Ruvuma, Mgambo JKT na Maramba JKT mkoani Tanga, Makuyuni JKT na Oljoro JKT mkoani Arusha, Bulombora JKT, Kanembwa JKT na Mtabila JKT mkoani Kigoma, Itaka JKT mkoani Songwe, Luwa JKT na Milundikwa JKT mkoani Rukwa, Nachingwea JKT mkoani Lindi pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) Kimbiji jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) wametakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwahudumia.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mabena ameeleza vifaa muhimu ambavyo vijana wanapaswa kwenda navyo kambini, vikiwemo bukta ya rangi ya dark blue yenye mpira kiunoni, mfuko mmoja wa nyuma, isiyo na zipu na yenye urefu unaoishia magotini, T-shirt ya kijani pamoja na raba za michezo za rangi ya kijani au bluu.
Vifaa vingine ni mashuka mawili ya rangi ya bluu bahari, soksi ndefu nyeusi, tracksuit ya rangi ya kijani au bluu, pamoja na nguo za kujikinga na baridi kwa wale waliopangiwa katika mikoa yenye hali ya hewa ya baridi.
Pia amewataka vijana kuhakikisha wanakwenda na nyaraka zote muhimu zitakazohitajika katika udahili wa elimu ya juu, zikiwemo cheti cha kuzaliwa, cheti cha kuhitimu kidato cha nne pamoja na nyaraka nyingine muhimu.
Brigedia Jenerali Mabena ameongeza kuwa orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, makambi waliyopangiwa, maeneo ya makambi hayo pamoja na mahitaji yote muhimu yanapatikana kupitia tovuti rasmi ya JKT.
Ends

0 Comments