WAKILI YOYO ASUBUHI AZINDUA JENGO JIPYA ARUMERU, ASISITIZA NGUVU YA IMANI KWA MUNGU
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
WAKILI maarufu mkoani Arusha, Yoyo Asubuhi, amezindua rasmi jengo jipya lililopo eneo la Olosiva, Kata ya Olorien, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, katika hafla kubwa ya shukrani iliyohudhuriwa na mamia ya wageni waalikwa wakiwemo viongozi wa dini, ndugu, marafiki pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Katika hafla ya kuweka wakfu jengo hilo litakalotumika kwa shughuli za biashara ya hoteli na huduma za malazi kwa wageni, iliyoongozwa na Mchungaji Gerald Nyakrere wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mwenge jijini Dar es Salaam jana, waumini, ndugu na marafiki walikusanyika kushuhudia tukio hilo muhimu lililoambatana na maombi maalum ya kuliombea jengo pamoja na shughuli zitakazofanyika ndani yake.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na maombi, nyimbo za shukrani na ibada maalum ya kuliombea jengo hilo, Wakili Yoyo alisema mafanikio ya mradi huo yametokana na kumweka Mungu mbele tangu hatua za mwanzo za ujenzi hadi kukamilika kwake.
Alisema jengo hilo si tu ishara ya mafanikio ya kimaendeleo, bali pia ni ushuhuda wa nguvu ya imani, maombi na mshikamano wa kiroho katika kufanikisha malengo makubwa ya maisha.
“Jengo hili tumelianza na Mungu na tutaendelea na Mungu. Tunaamini litakuwa sehemu ya baraka kwa watu wengi na chombo cha kumtukuza Mwenyezi Mungu katika kila hatua,” alisema Wakili Yoyo huku akipokea pongezi kutoka kwa wageni waliohudhuria hafla hiyo.
Alifafanua kuwa mradi huo ulianza rasmi Aprili 22, 2024, ambapo katika hatua ya uwekaji wa msingi aliwaalika viongozi wa kiroho kufanya ibada maalum ya kulibariki eneo hilo kabla ya kuanza kwa shughuli za ujenzi.
Kwa mujibu wa Wakili Yoyo, viongozi wa dini walioshiriki maombi hayo waliweka msingi wa kiroho ulioleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Mchungaji Gerald Nyakrere alisisitiza umuhimu wa kumshirikisha Mungu katika mipango ya maendeleo na maisha ya kila siku, akieleza kuwa mafanikio ya kweli huanzia kwenye msingi wa kiroho na uaminifu kwa Mungu.
“Mafanikio ya kweli huanzia kwenye msingi wa kiroho. Kumweka Mungu mbele ni siri ya ushindi katika kila jambo,” alisema Mchungaji Nyakrere wakati wa ibada ya kuweka wakfu jengo hilo.
Aidha, Wakili Yoyo alisema katika kipindi chote cha ujenzi amekuwa akiendesha shughuli hizo kwa maombi na usimamizi wa karibu, akiamini kuwa mafanikio ya kimwili hayawezi kutenganishwa na msingi imara wa kiimani.
Aliwahimiza wananchi kuendelea kuwa na moyo wa kumtumainia Mungu katika shughuli zao za kila siku, akisema kuwa amani, mafanikio na ustawi wa kweli hupatikana kupitia imani na bidii.
Katika hafla hiyo pia, Meneja wa Pamoja Microfinance Limited, Madam Glori Kipuyo, alitumia nafasi hiyo kueleza dhamira ya taasisi yao katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia huduma za mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Alisema taasisi hiyo imeendelea kusaidia makundi mbalimbali kukuza biashara zao na kuboresha maisha yao kupitia huduma rafiki za kifedha.
“Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa mitaji itakayowasaidia kukuza biashara zao na kufikia ndoto zao,” alisema Madam Kipuyo.
Aliongeza kuwa ofisi za Pamoja Microfinance Limited zinapatikana Kaloleni jijini Arusha, katika jengo la TUTA ghorofa ya pili karibu na Rushida Supermarket.
Kwa upande wake, familia ya Wakili Yoyo ilitoa shukrani za dhati kwa viongozi wa kanisa, walimu wa watoto, ndugu, marafiki pamoja na waumini wote walioshiriki kwa namna mbalimbali katika safari ya ujenzi wa jengo hilo.
...Ends..






0 Comments