SERIKALI, ICHA AFRICA WAUNGANA KUPAMBANA NA VIFO VYA WATOTO NJITI,WATAALAMU WA AFYA KUTOKA NCHI 22 WAKUTANA ARUSHA

 SERIKALI, ICHA AFRICA WAUNGANA KUPAMBANA NA VIFO VYA WAZAZI NA WATOTO NJITI

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA, 

SERIKALI imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya uliowezesha kupungua kwa kasi ya vifo vya wajawazito nchini, huku ikieleza kuwa juhudi zaidi zinaendelea kufanyika kukabiliana na vifo vya watoto wachanga hususan watoto njiti.


Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Arusha, Dkt. Prosper Mushi, wakati wa kongamano la kimataifa la “Tiny Feet Big Steps 2026” lililoandaliwa na taasisi ya Institute of Child Health Care Africa (ICHA Africa) jijini Arusha.


Dkt. Mushi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepata mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya wajawazito, hatua iliyomuwezesha Rais kutunukiwa tuzo maalum kutokana na mafanikio hayo.


“Karibuni Mheshimiwa Rais alitunukiwa tuzo kwa kuwa Rais wa kwanza kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya wajawazito ndani ya muda mfupi. Hii inaonesha namna Serikali ilivyojipanga kuimarisha sekta ya afya,” alisema Dkt. Mushi.


Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado ipo changamoto ya vifo vya watoto wachanga, hasa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao, jambo ambalo Serikali inaendelea kulipa kipaumbele kupitia uwekezaji katika mafunzo kwa wataalamu wa afya, uboreshaji wa miundombinu pamoja na vifaa tiba vya kisasa.


Kwa mujibu wa Dkt. Mushi, Serikali imeendelea kusambaza vifaa muhimu katika vituo vya afya ikiwemo mashine za kusaidia upumuaji kwa watoto wachanga (CPAP Machine), incubators, baby warmers pamoja na vifaa vingine vya kisasa.


Aidha, aliipongeza ICHA Africa kwa kushirikiana na Serikali katika jitihada za kuboresha afya ya mama na mtoto, akieleza kuwa wadau wa maendeleo ni nguzo muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.


“Tunatambua wadau wa maendeleo ni mkono wa pili wa Serikali. Ushirikiano kati ya Serikali na ICHA Africa utasaidia kuongeza kasi ya kuboresha afya ya kina mama na watoto wachanga,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa ICHA Africa, Robin Mwanga, alisema taasisi hiyo imekuwa ikiendesha kongamano la “Tiny Feet Big Steps” jijini Arusha kwa takribani miaka sita, likiwa na lengo la kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi wanaohudumia watoto njiti.


Mwanga alisema kongamano hilo limeendelea kupata umaarufu mkubwa barani Afrika kiasi cha kuanza kualikwa katika mataifa mbalimbali ikiwemo Ethiopia, Uganda na Ghana.


“Kila mwaka tunafanya conference hii hapa Arusha, lakini sasa mataifa mengine yameona umuhimu wake na kuanza kutualika kwenda kufanya mafunzo haya katika nchi zao,” alisema Mwanga.


Alifafanua kuwa Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vitengo maalum vya uangalizi wa watoto wachanga mahututi (Neonatal Intensive Care Unit - NICU), huku akibainisha kuwa Mkoa wa Arusha bado una Neonatal Care Unit lakini haujapata Neonatal Intensive Care Unit kamili.


Mwanga alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa afya ili waweze kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya muda kwa ufanisi zaidi na kupunguza vifo vya watoto hao.


“Tunataka kupunguza vifo vya watoto hawa njiti na kuwapa wazazi matumaini kwamba hata mtoto aliyezaliwa kabla ya muda bado anaweza kuishi na kuwa na afya njema,” alisema.


Aliongeza kuwa mafunzo hayo hayaishii katika tiba pekee, bali pia yanajumuisha namna ya kuwasaidia wazazi kisaikolojia ili waweze kuwapokea na kuwalea watoto wao bila kukata tamaa.


“Wazazi wengi wanakata tamaa wanapopata mtoto ambaye hajatimiza wiki 40 za ujauzito, lakini kitu kikubwa ni kuwajengea moyo wa kumkubali mtoto wao na kujenga ukaribu naye,” alisema.


Mwanga alisema moja ya mifumo muhimu inayosisitizwa katika huduma za watoto njiti ni Kangaroo Mother Care (KMC), mfumo unaomwezesha mama kumbeba mtoto karibu na mwili wake ili kumpatia joto, kujenga ukaribu na kusaidia ukuaji wake.


Katika kongamano hilo la mwaka huu, wataalamu kutoka nchi 22 duniani walishiriki kwa ajili ya mafunzo, kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu mbalimbali za kuboresha huduma za watoto wachanga.


Kutokana na mafanikio hayo, Mwanga alisema mwaka huu ICHA Africa inatarajia kufanya makongamano kama hayo nchini Uganda mwezi Oktoba na Ghana mwezi Novemba.


Kwa upande wake, Dkt. Mushi alisema Mkoa wa Arusha umeendelea kufanya vizuri katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ingawa bado zipo changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa Serikali, wataalamu wa afya na jamii.


Alisema baadhi ya changamoto hizo zinatokana na mazingira ya kijamii, uhitaji wa mafunzo zaidi kwa wataalamu pamoja na upatikanaji wa huduma bora katika baadhi ya maeneo.


Watoa mada hao waliwahimiza madaktari, wauguzi na wadau wa afya nchini kutumia fursa ya kongamano hilo kuongeza ujuzi na kuimarisha huduma kwa watoto wachanga ili kuendelea kuokoa maisha ya kina mama na watoto nchini.







ENDS .

Post a Comment

0 Comments