WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NA ULEVI WA POMBE

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NA ULEVI WA POMBE 

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

AFISA Mradi kutoka Shirika la Blue Cross Society of Tanzania, Glory Vincent Pagundile, amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya, pombe na tumbaku kupitia utoaji wa elimu sahihi kwa jamii.

Glory aliyasema hayo jijini Arusha katika semina na waandishi wa habari iliyoandaliwa na shirika hilo chini ya mpango wa Afya kwa vijana na jamii,Zuia Madhara yanayotokana na dawa za kulevya na pombe,iliyolenga kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kampeni za utoaji elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya pamoja na changamoto zinazoendelea kuikabili jamii ikiwemo ukatili unaotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema bado ipo haja kubwa ya kuongeza elimu kwa wananchi kwani vijana wengi wanaendelea kuathirika kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo.

“Waandishi wa habari ni kiungo muhimu sana katika mapambano haya. Kupitia kalamu zao wana uwezo mkubwa wa kuelimisha jamii na kusaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao,” alisema Glory.

Alieleza kuwa Blue Cross Society of Tanzania imejikita katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya, pombe, tumbaku pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari.



Kwa mujibu wa Glory, shirika hilo linaamini kuwa elimu inayotolewa kupitia redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii ina uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja tofauti na elimu inayotolewa katika maeneo machache ya mikutano au madarasa.

“Tunapoingia kwenye vyombo vya habari tunapata nafasi ya kuwafikia watu wengi zaidi. Ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na waandishi wa habari ili kuhakikisha taarifa sahihi zinaifikia jamii kwa wakati,” alisema.

Aidha alisema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi zinazohusu matumizi ya dawa za kulevya pamoja na uwepo wa mitazamo hasi na baadhi ya tamaduni zinazochangia kuendelea kwa tatizo hilo katika jamii.


Aliongeza kuwa wakati mwingine vitendo vya rushwa na uzembe wa baadhi ya watu vinachangia elimu na taarifa sahihi kutowafikia wananchi ipasavyo.

“Hivyo tunaziomba mamlaka husika kuendelea kusimamia kwa karibu mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pombe na tumbaku ili kuokoa nguvu kazi ya taifa hasa vijana,” alisema.

Glory alisema pamoja na changamoto hizo, shirika hilo limeanza kuona matokeo chanya kupitia kampeni zake za elimu ambapo baadhi ya vijana waliokuwa katika hatari ya kuanza matumizi ya dawa za kulevya wamebadili mitazamo yao baada ya kupata elimu.

Alisema pia baadhi ya waliokuwa tayari wameathirika wameonyesha mabadiliko na kuamua kuacha matumizi ya dawa hizo baada ya kupata elimu na ushauri.

Katika hatua nyingine, alisema shirika hilo limefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 20,000 kupitia kampeni mbalimbali za elimu, mafunzo kwa viongozi wa kata na mitaa pamoja na vijana wanaopewa elimu rika ili nao wawe mabalozi wa kuelimisha wenzao.

“Tunawajengea uwezo vijana ili waweze kutoa elimu kwa vijana wengine. Tunaamini njia hiyo itasaidia ujumbe kufika kwa watu wengi zaidi na kusaidia kupunguza madhara ya dawa za kulevya kwenye jamii,” alisema.

Alisisitiza kuwa Blue Cross Society of Tanzania itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari pamoja na taasisi mbalimbali kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi itakayosaidia kujenga taifa lenye vijana wenye maadili na afya bora.

**ends**

Post a Comment

أحدث أقدم