UBOVU WA BARABARA WAITESA LONGIDO WANANCHI,WAJAWAZITO WATUMIA PUNDA KWENDA KUJIFUNGUA,WENGI WAJIFUNGULIA PORINI,SERIKALI YAOMBWA KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA KUBIRESHA MIUNDOMBINU.

  BARABARA MBOVU LONGIDO ZAWATESA WAJAWAZITO, WANANCHI WATUMIA PUNDA KWENDA KUJIFUNGUA

Na Joseph Ngilisho|LONGIDO

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Thomas Ngobei, ameitaka Serikali kuongeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya barabara baada ya maeneo mbalimbali kuharibiwa vibaya na mvua za masika huku wananchi wakilazimika kutumia usafiri wa punda kuwapeleka wajawazito hospitalini na baadhi yao kujifungulia njiani kutokana na barabara kutopitika kabisa kwa vyombo vya moto.

Ngobei alitoa kauli hiyo baada ya kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo alisema changamoto kubwa iliyojitokeza ni hali mbaya ya barabara katika kata za Elang'atadapash na Ilorienito zilizokatika mawasiliano kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni.

Alisema hali hiyo imekuwa ikihatarisha maisha ya wananchi hasa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka za matibabu.






“Kwa sasa kuna changamoto kubwa katika kata za Elang'atadapash na Ilorienito. Barabara nyingi hazipitiki kabisa kwa asilimia 100 kutokana na mvua za masika. Wananchi wanatumia punda kuwapeleka wajawazito hospitalini na wengine wanajifungulia njiani kwa sababu magari hayawezi kupita,” alisema Ngobei.

"Tunaomba wenzetu wa Tarura wapite katika kata zote ili waangalie namna ya kurejesha mtandao wa barabara katika halmashauri yetu"

Aidha alisema barabara inayotoka Kitumbeine kuelekea Elang'atadapash imekatika kabisa jambo lililosababisha wananchi kushindwa kupata huduma muhimu kwa urahisi.

Kutokana na hali hiyo, baraza la madiwani limeiomba Serikali pamoja na TARURA kuchukua hatua za dharura kurejesha mawasiliano katika maeneo yaliyoathirika ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii na kiuchumi bila usumbufu.

Katika hatua nyingine, Ngobei alisema halmashauri hiyo imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo hadi sasa imefikisha asilimia 78 ya lengo huku wakitarajia kufikia asilimia 100 kabla ya mwisho wa mwezi Juni.

Aliwataka wananchi na wafanyabiashara wa Wilaya ya Longido kuwa waaminifu katika kulipa kodi ili kuongeza mapato yatakayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia baraza hilo limesisitiza umuhimu wa taasisi za Serikali zikiwemo TANESCO, RUWASA na TARURA kushiriki katika vikao vya kamati za halmashauri ili kurahisisha mipango ya maendeleo katika sekta za elimu, maji, umeme na barabara.

Sambamba na hayo, halmashauri hiyo imewataka wananchi kushiriki katika nguvu kazi ya jamii kwa ajili ya kufanya matengenezo ya muda mfupi katika maeneo yanayoweza kufikika wakati wakisubiri msaada mkubwa kutoka TARURA.


Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم