TAPSEA WALALAMIKA KUDHALILISHWA MITANDAONI
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi na Waendesha Ofisi Tanzania Bara na Zanzibar (TAPSEA), Zuhura Maganga, amelalamikia vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa dhidi ya waandishi na waendesha ofisi kupitia mitandao ya kijamii, akisema vinaendelea kushusha hadhi ya taaluma hiyo muhimu katika utumishi wa umma
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa 13 wa TAPSEA, Maganga alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii, hususan Instagram, kuonesha kada ya waandishi na waendesha ofisi kama kada isiyo na maadili, jambo ambalo si sahihi
Alisema waandishi na waendesha ofisi wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika uratibu wa shughuli za viongozi, usimamizi wa taarifa, mawasiliano ya taasisi pamoja na kuhakikisha shughuli za ofisi zinaenda kwa ufanisi mkubwa.
“Hawa ni wataalamu waliopata mafunzo rasmi ya Serikali na wana mchango mkubwa katika mafanikio ya taasisi mbalimbali nchini,” alisisitiza.
Maganga alisema TAPSEA itaendelea kusimamia na kutetea hadhi ya kada hiyo ili jamii iweze kuitambua kwa heshima inayostahili.
Katika hatua nyingine, alisema chama hicho kinaendelea kujiimarisha kiuchumi kupitia uwekezaji wa mali za chama ambapo tayari kimefanikiwa kupata viwanja viwili kwa ajili ya kujenga ofisi za kudumu pamoja na vitega uchumi vitakavyoongeza mapato ya taasisi.
“Hatua hii inaonesha dhamira ya TAPSEA kujitegemea kifedha na kuimarisha maendeleo ya chama chetu. Tunaomba Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kutuunga mkono katika uwekezaji huu,” alisema.
Aidha, Maganga alisema TAPSEA inajivunia mafanikio ya kukuza taaluma ya waandishi na waendesha ofisi kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Hata hivyo, alieleza kuwa bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili taaluma hiyo, ikiwemo upungufu wa vifaa vya kufundishia katika vyuo vya mafunzo ya uandishi na uendeshaji wa ofisi.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa kompyuta, madawati, mashine za uchapaji (typewriter) pamoja na vifaa vya kisasa vya TEHAMA vinavyohitajika katika kujifunza kwa ufanisi.
Pia alisema kuna uhaba wa walimu wabobezi wenye utaalamu maalumu katika kada hiyo, hali inayokwamisha jitihada za kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
“Tunahitaji mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ili kuendana na kasi ya dunia ya kidijitali na kuongeza ushindani wa wataalamu wetu katika soko la ajira,” alisema.
Maganga alisisitiza kuwa ofisi ni sehemu ya kazi na si mahali pa kudhalilisha taaluma za watu, huku akiwataka Watanzania kuthamini mchango wa waandishi na waendesha ofisi katika maendeleo ya nchi.
**Ends**





إرسال تعليق