Na Joseph Ngilisho – Arusha
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amesema Tanzania imejipanga kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Urusi na mataifa mengine duniani kwa lengo la kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.
Dkt. Chaya alisema hayo jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililowakutanisha zaidi ya kampuni 120 kutoka Urusi pamoja na wadau wa sekta binafsi na serikali kutoka Tanzania.
Katika hotuba yake leo May 15,2026, aliwashukuru Wizara ya Maendeleo ya Uchumi ya Urusi, Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania, Russia Congress Foundation, Russian Export Center, Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Zanzibar Investment Promotion Agency (ZIPA), Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) pamoja na wadau wengine kwa kuandaa kongamano hilo muhimu lenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi.
Alisema kongamano hilo limekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya nchi kuwa uchumi wa kisasa unaotegemea viwanda, teknolojia, ubunifu na ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi.
“Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi makubwa ya uchumi chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambapo serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya mazingira ya biashara, kuimarisha miundombinu na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje,” alisema Dkt. Chaya.
Alisema Tanzania ina nafasi muhimu kimkakati kutokana na kuwa lango la soko la zaidi ya watu milioni 300 kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), jambo linaloifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.
Aidha alisema Arusha, ambako kongamano hilo limefanyika, linaendelea kujizolea sifa kama “Geneva ya Afrika” kutokana na mchango wake katika diplomasia, mazungumzo ya amani na ushirikiano wa kimataifa, sambamba na kuwa lango la vivutio vikubwa vya utalii duniani ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Tarangire na Ziwa Manyara.
Dkt. Chaya alisema serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA), ZIPA pamoja na vituo vya huduma kwa wawekezaji vya One Stop Facilitation Centre vinavyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji.
Alitaja sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji kuwa ni pamoja na madini, viwanda, kilimo cha kisasa, mbolea, nishati, TEHAMA, usafirishaji, anga, dawa, utalii pamoja na uhamishaji wa teknolojia.
“Tunawaalika wawekezaji wa Urusi kuja kuwekeza Tanzania na kuwa sehemu ya safari yetu ya mageuzi ya uchumi. Tanzania ni nchi yenye utulivu wa kisiasa, sera rafiki za uwekezaji, rasilimali nyingi na soko linalokua kwa kasi,” alisema.
Aliongeza kuwa ushiriki wa zaidi ya kampuni 120 kutoka Urusi unaonesha kuongezeka kwa imani ya sekta binafsi ya Urusi katika mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Dkt. Chaya alieleza kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa kongamano hilo litafungua njia mpya za biashara, uwekezaji, ushirikiano wa utalii, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya pamoja kati ya Tanzania na Urusi.
Ends..





0 Comments