SERIKALI YAJIVUNIA MCHANGO WA CRDB KATIKA KUCHOCHEA UCHUMI,VIJANA WAHIMIZWA KUMILIKI UCHUMI KUPITIA UWEKEZAJI WA HISA

SERIKALI YAJIVUNIA MCHANGO WA CRDB KATIKA KUCHOCHEA UCHUMI,VIJANA WAHIMIZWA KUMILIKI UCHUMI KUPOTIA UWEKEZAJI WA HISA 

 Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

SERIKALI imesema inajivunia uwepo wa CRDB Bank Plc kwa kuendelea kuimarisha jitihada za Serikali za kuunganisha akiba za wananchi, mitaji ya uwekezaji na mahitaji ya maendeleo ya kiuchumi, huku takribani asilimia 29 ya mikopo yote ya sekta binafsi nchini ikitolewa na benki hiyo.

Kauli hiyo imetolewa May 15,2026 na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa CRDB Bank  iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 31 wa mwaka wa benki hiyo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), chini ya kaulimbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa.”


Waziri Omar alisema Serikali inaendelea kuipongeza benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha uwekezaji nchini, hususan kwa vijana kupitia elimu ya fedha, uwekezaji wa hisa na programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi zinazolenga kujenga kizazi kipya cha wawekezaji wa Kitanzania.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu imebeba ujumbe mkubwa wa kimkakati kwa Taifa kwani vijana hawapaswi kuendelea kuwa watafuta ajira pekee, bali wanapaswa kushiriki kikamilifu katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.

“Vijana ni nguvu kubwa ya uchumi wetu kutokana na idadi yao kubwa nchini. Tukiwajengea uelewa wa uwekezaji mapema, tutakuwa tunajenga Taifa lenye uchumi imara, jumuishi na shindani,” alisema Waziri Omar.

Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuimarisha sekta ya fedha ili kuwapa wananchi, hasa vijana, fursa pana za kushiriki katika uchumi kupitia uwekezaji wa hisa, hati fungani na mifuko ya uwekezaji.

Katika hotuba yake, Waziri huyo alisema thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji nchini imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 47.2 mwaka 2024 hadi trilioni 63.1 mwaka 2025, huku mauzo ya hisa na dhamana yakiongezeka kwa asilimia 91, jambo alilosema linaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji nchini.

Aidha, alisema sekta ya benki nchini imeendelea kuimarika kwa kasi ambapo mali za sekta hiyo zimeongezeka kutoka Shilingi trilioni 39.3 mwaka 2021 hadi trilioni 77 mwaka 2025, huku kiwango cha mikopo chechefu kikishuka kutoka asilimia 5.8 hadi asilimia 2.8.

Waziri Omar aliipongeza pia CRDB Bank Plc kwa kuendelea kuwa mfano wa taasisi inayochochea ushiriki wa wananchi katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.

Alisema mafanikio ya benki hiyo yameifanya kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Taifa, huku akiisifu kwa kupanua huduma zake nje ya Tanzania kupitia uwepo wake Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na mipango ya kuingia Kenya na Zambia.

Pia aliipongeza benki hiyo kwa hatua yake ya kufungua Ofisi ya Uwakilishi Dubai, akisema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa historia katika sekta ya fedha nchini na kuiweka Tanzania katika jukwaa la kimataifa la fedha na uwekezaji.

“Hatua hii inaonyesha maono mapana, ujasiri wa taasisi na imani kubwa katika uwezo wa Watanzania kushindana katika soko la kimataifa,” alisema Waziri huyo.

Kwa mujibu wa Waziri Omar, CRDB Bank Plc imeendelea kufanya vizuri kibiashara baada ya kupata faida safi ya Shilingi bilioni 725 mwaka 2025 baada ya kodi, jambo lililoifanya kuendelea kuwa moja ya taasisi kubwa za kifedha Afrika Mashariki na Kati.

Katika semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank ,Dkt  Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwawezesha vijana kupitia huduma za kifedha, ubunifu, elimu ya uwekezaji na programu za maendeleo ya ujasiriamali.

Alisema kupitia CRDB Bank Foundation pamoja na programu ya IMBEJU, benki hiyo imefanikiwa kuwafikia maelfu ya vijana na biashara changa kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na fursa za kukuza biashara zao.

“Tunaamini vijana wa leo si wateja tu wa benki yetu, bali ndiyo wawekezaji, wabunifu na viongozi wa uchumi wa kesho. Ndiyo maana tunataka wawe sehemu ya safari ya ukuaji wa taasisi yetu na uchumi wa Taifa,” alisema Dkt. Nsekela.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc, Neema Mori alisema uwekezaji katika hisa ni moja ya njia muhimu za kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu kwa vijana na familia za Kitanzania.

Profesa Mori alisema CRDB Bank  ni ushahidi hai wa namna uwekezaji wa muda mrefu unavyoweza kubadilisha maisha ya watu, akieleza kuwa wanahisa wengi waliowekeza zaidi ya miaka 30 iliyopita sasa wanashuhudia matokeo ya maamuzi yao ya kimkakati.

“Leo tunajivunia kuona CRDB ikiwa taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini na moja ya taasisi kubwa za kifedha Afrika Mashariki na Kati. Ukuaji huu umeambatana na ongezeko kubwa la thamani ya uwekezaji wa wanahisa wetu,” alisema Profesa Mori.

Alieleza kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita, thamani ya hisa za benki hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 253, huku hisa zake zikifikia wastani wa Shilingi 2,800 kutoka Shilingi 460 mwaka 2023.

Aidha, alisema Bodi ya Wakurugenzi itawasilisha pendekezo la gawio la Shilingi 90 kwa kila hisa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha ya mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Profesa Mori pia aliwahamasisha wazazi na familia kuanza kujenga utamaduni wa uwekezaji mapema kwa watoto wao kwa kuwawekezea hisa, hatua aliyosema inaweza kuwa msingi wa usalama wa kifedha kwa kizazi kijacho.

Semina hiyo ya wanahisa iliwakutanisha viongozi wa Serikali, wanahisa, wataalamu wa masoko ya mitaji, vijana pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha kujadili nafasi ya vijana katika uwekezaji na mustakabali wa uchumi wa Taifa kupitia masoko ya mitaji.








Ends..

Post a Comment

0 Comments