TANZANIA NA URUSI ZAFUNGUA UKURASA MPYA WA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI, ELIMU NA NISHATI

 TANZANIA NA URUSI ZAFUNGUA UKURASA MPYA WA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI, ELIMU NA NISHATI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi zimefungua rasmi ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta za kiuchumi, elimu, nishati, afya na miundombinu, kufuatia mazungumzo ya kina yaliyofanyika kwa siku kadhaa yakihusisha viongozi wa serikali, taasisi na sekta binafsi kutoka pande zote mbili.

Mazungumzo hayo yalihitimishwa kupitia Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi lililofanyika Arusha, likiwakutanisha wawekezaji, wafanyabiashara na watunga sera kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kufungua fursa mpya za uwekezaji.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano 12 ,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia mitaji zaidi kutoka nje na ndani ya nchi, huku akisisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Urusi katika sekta mbalimbali.

Pande hizo mbili zimekubaliana kuendeleza utekelezaji wa mikataba ya ushirikiano iliyosainiwa mwaka 2022, sambamba na kuandaa mikataba mipya itakayogusa sekta za kilimo, nishati, elimu, afya, utalii na miundombinu.

Baadhi ya mikataba hiyo tayari imeshasainiwa, huku mingine ikitarajiwa kusainiwa jijini Moscow wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, inayotarajiwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu.

Katika sekta ya elimu na utamaduni, makubaliano yamefikiwa ya kuimarisha ufundishaji wa lugha, ambapo Kiswahili kitaanza kufundishwa katika vyuo vikuu sita vya Urusi, huku lugha ya Kirusi nayo ikifundishwa katika taasisi za elimu nchini Tanzania.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha urafiki wa muda mrefu na kuongeza uelewa wa kijamii na kitamaduni kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Pia imeelezwa kuwa zaidi ya Watanzania 20,000 wamenufaika na ufadhili wa masomo nchini Urusi katika nyanja mbalimbali, na mpango wa kuongeza nafasi zaidi kwa vijana unaendelea kuimarishwa.

Katika sekta ya afya, Tanzania na Urusi zimekubaliana kushirikiana katika utoaji wa huduma za afya na uzalishaji wa dawa kupitia taasisi mbalimbali.

Kwa upande wa kilimo, Urusi imeahidi kuendelea kusambaza mbolea, teknolojia za kisasa za kilimo, mbegu bora na mifumo ya kuongeza tija ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya Tanzania kabla ya mauzo ya nje.

Aidha, mpango wa kuanzisha uzalishaji wa vifaa vya afya kama rapid test kits nchini Tanzania umepangwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Sekta ya nishati imeelezwa kuwa mhimili muhimu wa ushirikiano huo, ambapo makampuni ya Urusi yameonyesha nia ya kuwekeza katika utafutaji, uchimbaji na biashara ya gesi asilia nchini Tanzania.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi asilia, ambao tayari ni sehemu kubwa ya nishati ya taifa.

Aidha, miradi ya kimkakati kama Mkuju River, inayohusisha uchimbaji wa uraniamu, imeendelea kupewa kipaumbele katika mazungumzo hayo.

Katika miundombinu, wawekezaji wa Urusi wameonyesha nia ya kushiriki katika upanuzi na ujenzi wa bandari pamoja na kuboresha mifumo ya usafirishaji wa mizigo nchini.

Ushirikiano kati ya mamlaka za bandari za Tanzania na kampuni za Urusi unalenga kuongeza ufanisi wa biashara na kupunguza gharama za usafirishaji.

Sekta ya utalii imeendelea kuwa daraja muhimu la ushirikiano, ambapo Urusi ni moja ya masoko yanayokua kwa kasi ya watalii wanaotembelea Tanzania.

Taarifa zinaeleza kuwa Shirika la Ndege la Taifa, Air Tanzania Company Limited, linatarajia kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kuelekea Moscow, hatua itakayoongeza mtiririko wa watalii na wawekezaji.

Zaidi ya watalii 17,000 kutoka Urusi walitembelea Tanzania mwaka 2025, huku ikitarajiwa idadi hiyo kuongezeka kwa kasi kutokana na kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Maksim Reshetnikov, amesema Urusi ipo tayari kuongeza uwekezaji mkubwa nchini Tanzania katika sekta za kilimo, nishati, viwanda, utalii na miundombinu.

Amesema biashara kati ya nchi hizo mbili imeongezeka kwa takriban asilimia 20 ndani ya mwaka mmoja, huku Urusi ikiendelea kusafirisha bidhaa kama ngano, mbolea na bidhaa za viwandani, na kuagiza mazao ya Tanzania ikiwemo kahawa, chai, korosho na matunda.


Ends .

Post a Comment

0 Comments