DKT. LUKUMAY AITAKA AFRIKA KUONGEZA FEDHA ZA NDANI KUPAMBANA NA KIFUA KIKUU
Na Joseph Ngilisho|ARUSHADIGITAL
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMWI, Johannes Lembulung Lukumay, anashiriki Mkutano wa Wenyeviti wa Kamati za Afya na Fedha wa nchi zinazozungumza Kiingereza barani Afrika kuhusu Global TB Caucus unaofanyika kuanzia Mei 14 hadi 15, 2026 jijini Cape Town.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa mabunge, wataalamu wa afya na watunga sera kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kujadili namna ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB), UKIMWI na malaria kupitia mifumo endelevu ya ufadhili wa sekta ya afya.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Lukumay alisema kuwa Global TB Caucus inalenga kusaidia nchi mbalimbali kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa misaada ya wahisani wa kimataifa katika programu za kifua kikuu, huku ikihamasisha ongezeko la fedha za ndani kwa ajili ya sekta ya afya.
Alisema jukwaa hilo pia lina jukumu muhimu la kushawishi sera na mipango ya kifedha ya serikali hasa katika kipindi cha maandalizi ya bajeti za Februari hadi Machi 2026, ili kuhakikisha ugonjwa wa TB unapewa kipaumbele stahiki katika mgao wa rasilimali za afya.
“Global TB Caucus ni muhimu katika kuendeleza shinikizo la kisiasa la kutokomeza kifua kikuu, kwani makundi ya kitaifa ya wabunge ndiyo msingi wa utetezi wa TB katika ngazi za kikanda na kimataifa,” alisema Dkt. Lukumay.
Katika uwasilishaji wake, Dkt. Lukumay alieleza kuwa Tanzania bado ipo miongoni mwa nchi 30 duniani zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa wa kifua kikuu kulingana na takwimu za World Health Organization, ingawa kiwango cha maambukizi kimeendelea kupungua.
Alisema kufikia mwaka 2023, wastani wa maambukizi ya TB nchini ulikuwa umefikia wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000, hali inayoonesha mafanikio ya juhudi zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wa afya katika kudhibiti ugonjwa huo.
Hata hivyo, Dkt. Lukumay alibainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa katika upatikanaji wa fedha za matibabu na vifaa vya uchunguzi wa TB. Kutokana na hali hiyo, aliitaka Global TB Caucus kusaidia kutetea kupunguzwa kwa bei za dawa za TB pamoja na vifaa vya maabara kutoka kwa wazalishaji wa kimataifa ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa nchi zinazoendelea.
Aidha, aliomba kuongezwa kwa kiwango cha fedha kinachotolewa kupitia Global Fund kwa ajili ya mapambano dhidi ya TB, akieleza kuwa kwa sasa ruzuku ya TB hupata asilimia saba pekee ikilinganishwa na fedha zinazotengwa kwa malaria na UKIMWI.
Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, hali hiyo imekuwa ikiathiri juhudi za kupambana na kifua kikuu licha ya ugonjwa huo kuendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wananchi katika nchi nyingi za Afrika.
Katika hitimisho lake, Dkt. Lukumay aliwataka wabunge kutoka nchi mbalimbali kushirikiana kutetea ongezeko la fedha za ndani kwa ajili ya mapambano dhidi ya TB, UKIMWI na malaria, akisisitiza kuwa serikali za Afrika zinapaswa kuongeza uwajibikaji katika kugharamia huduma za afya badala ya kutegemea zaidi misaada ya nje.
Ends .

0 Comments