TAKUKURU ARUSHA YAVUNJA MTANDAO WA NYARAKA FEKI, VIWANJA VYA SH. BILIONI 3 VYAREJESHWA SERIKALINI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imefanikiwa kuzuia uporaji wa viwanja vitatu vya thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3 baada ya kubaini matumizi ya nyaraka za kughushi katika mchakato wa kuhamisha umiliki wa mali hizo, hatua iliyosaidia kurejesha umiliki halali pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusu taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha miezi mitatu , Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, alisema mafanikio hayo yametokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na taasisi hiyo baada ya kubaini dalili za udanganyifu katika mchakato wa umilikishaji wa viwanja hivyo.
Ngailo alisema uchunguzi huo uliwezesha kubainika kwa uwepo wa nyaraka za uongo zilizokuwa zikitumika kuhamisha umiliki wa viwanja hivyo kinyume cha sheria na taratibu za ardhi.
“Mfumo wa uchunguzi wetu umebaini uwepo wa mianya ya rushwa na matumizi ya nyaraka za kughushi yaliyokuwa yakihatarisha upotevu wa mali hizo. Kupitia ushirikiano wetu na taasisi nyingine za Serikali tumefanikiwa kurejesha viwanja hivyo kwa mmiliki halali,” alisema Ngailo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viwanja vilivyohusika ni Kiwanja Na. 1 Kitalu “D” pamoja na Viwanja Na. 5 na Na. 7 Kitalu “F” vilivyopo Kata ya Levolosi jijini Arusha, ambavyo kwa pamoja vina thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 3.
TAKUKURU ilisema uchunguzi wake ulibaini kuwa baadhi ya watu waliwasilisha nyaraka zenye taarifa za uongo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha pamoja na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Arusha kwa lengo la kubadilisha umiliki wa viwanja hivyo kinyume cha sheria na taratibu za ardhi.
Imeelezwa kuwa katika nyaraka hizo, thamani ya kila kiwanja ilionyeshwa kuwa Shilingi Milioni 500 pekee, tofauti na thamani halisi iliyokuwa takribani Shilingi Bilioni 1 kwa kila kiwanja, hali iliyotafsiriwa kuwa njama za kukwepa kodi na kuhalalisha uhamisho usiofuata sheria.
Baada ya kubaini udanganyifu huo, TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi pamoja na Halmashauri ya Jiji la Arusha ilichukua hatua za haraka kurejesha hati zote tatu katika hali yake ya awali na kuhakikisha viwanja hivyo vinabaki chini ya msimamizi halali wa mirathi.
Katika hatua nyingine iliyotajwa kuwa ushindi mkubwa kwa Serikali, TAKUKURU ilieleza kuwa baada ya kurekebishwa kwa umiliki huo, Kiwanja Na. 1 Kitalu “D” kiliuzwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria kwa thamani ya Shilingi Bilioni 2, jambo lililoifanya Serikali kunufaika kwa kupata mapato ya Shilingi Milioni 90 kupitia kodi na ada mbalimbali.
Mapato hayo yalijumuisha Shilingi Milioni 60 za Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gain Tax) zilizolipwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shilingi Milioni 15 za stempu pamoja na Shilingi Milioni 15 za ada za usajili wa hati.
Ngailo alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa dhidi ya vitendo vya rushwa, udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka, hasa katika sekta ya ardhi ambayo imekuwa ikikabiliwa na migogoro mingi inayotokana na nyaraka za kughushi na ubadhirifu.
Mbali na operesheni hiyo ya viwanja, taasisi hiyo pia imeendelea kusimamia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.
Katika kipindi hicho cha miezi mitatu, TAKUKURU Arusha ilifanya ukaguzi wa miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.6 kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kudhibiti mianya ya ubadhirifu.
Aidha, taasisi hiyo imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa ambapo zaidi ya wananchi na wadau 17,000 walifikiwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, maonesho ya kitaasisi pamoja na klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni.
Kwa upande wa uchunguzi wa makosa ya rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Arusha ilipokea jumla ya malalamiko 94 katika kipindi hicho, huku zaidi ya asilimia 70 ya malalamiko hayo yakihusiana moja kwa moja na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa kesi 18 za rushwa na uhujumu uchumi ziliendeshwa mahakamani katika kipindi hicho, ambapo Jamhuri ilifanikiwa kushinda kesi 10 zilizosaidia kuokoa fedha za umma zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 205.
TAKUKURU Mkoa wa Arusha imewahakikishia wananchi kuwa itaendelea kushirikiana nao katika vita dhidi ya rushwa na kuwataka kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia ofisi zake au kwa kutumia simu ya bure namba 113 ili kusaidia kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha haki inatendeka.
Ends .

Post a Comment