MBUNGE NDOINYO ATOA UJUMBE MZITO OLOIPIRI, ASISITIZA UMOJA NA MAENDELEO,WANANCHI WAJAWA NA MSISIMKO WA FURAHA KUMWONA!
Na Joseph Ngilisho| Arusha Digital-NGORONGORO
Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, ametoa ujumbe mzito kwa wananchi wa Kata ya Oloipiri akiwataka kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano kwa viongozi wao ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Ndoinyo ameyasema hayo leo Mei 27, 2026 aliposhiriki katika sherehe maalum iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Oloipiri, Mh. Latajeuwo Soyorri, kwa ajili ya kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pamoja na mambo mengine Mbunge Yanik aliwaomba wananchi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake kwa sababu ya mambo mengi mazuri anayofanya na atakayofanya Kwa wakazi wote wa Wilaya ya Ngorongoro.
Katika hotuba yake mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye sherehe hiyo, Mbunge huyo alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila mshikamano wa wananchi na viongozi wao, huku akisisitiza kuwa wananchi wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko chanya kupitia ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
“Maendeleo ya kweli yanajengwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wao. Leo nimefarijika kuona Oloipiri inaendelea kuwa mfano wa umoja na mshikamano. Hii ndiyo njia sahihi ya kufikia maendeleo endelevu,” alisema Ndoinyo.
Aidha, aliwapongeza wananchi wa Oloipiri kwa kuendelea kuwa karibu na viongozi wao na kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo, akisema hatua hiyo imechangia kuimarika kwa ustawi wa jamii na kuongeza matumaini ya maendeleo zaidi katika eneo hilo.
Mbunge huyo pia alimpongeza Diwani wa Kata ya Oloipiri, Mheshimiwa Latajeuwo Soyorri, kwa namna anavyoendelea kusimamia maslahi ya wananchi na kutekeleza majukumu yake kwa karibu na wananchi wake.
“Diwani huyu ameonyesha mfano mzuri wa uongozi wa kuwafuata wananchi na kusikiliza changamoto zao. Hii ndiyo aina ya viongozi wanaohitajika katika jamii yetu,” alisisitiza Ndoinyo.
Kwa upande wake, Diwani Latajeuwo Soyorri alisema sherehe hiyo imelenga kuimarisha mshikamano kati ya viongozi na wananchi pamoja na kutoa shukrani kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika Kata ya Oloipiri yametokana na ushirikiano wa wananchi, viongozi wa vijiji pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza kufurahishwa na uwepo wa Mbunge wao pamoja na kauli zake zilizosisitiza amani, umoja na maendeleo, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wao kwa ajili ya maendeleo ya kata hiyo na Wilaya ya Ngorongoro kwa ujumla.
Ends






Post a Comment