SERIKALI YAPIGA HATUA KUIMARISHA UTOAJI HAKI NCHINI, YASISITIZA MATUMIZI YA NJIA MBADALA ZA MIGOGORO YA KISHERIA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
SERIKALI imeendelea kupiga hatua kubwa katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini kupitia maboresho ya mifumo ya kisheria, ongezeko la ufanisi kwa mawakili wa serikali pamoja na kuimarika kwa matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), hususan katika migogoro ya ardhi, hatua inayolenga kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani na kuongeza kasi ya upatikanaji wa haki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo mawakili wa serikali jijini Arusha May 18,2026 Waziri wa Katiba na Sheria,dkt Juma Homera, alisema mageuzi hayo tayari yameanza kuleta matokeo chanya katika uendeshaji wa mashauri na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Alisema mawakili wa serikali wameendelea kuonesha ufanisi mkubwa katika kulinda maslahi ya taifa kupitia usimamizi makini wa kesi mbalimbali, sambamba na kuimarika kwa matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwemo usuluhishi.
“Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya haki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, hususan katika maeneo ya migogoro ya ardhi ambayo yamepewa kipaumbele maalum,” alisema Waziri Homera.
Aidha, alikemea vikali matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayotumiwa na baadhi ya watu kuichafua serikali na kusababisha taharuki kwa jamii, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria.
Alielekeza vyombo vya dola na mawakili wa serikali kusimama kidete katika kuhakikisha uhalifu wa mtandaoni unadhibitiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria, huku akiwataka washiriki wa mafunzo hayo kuongeza weledi, maadili na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, aliwataka mawakili wa serikali kuongeza weledi na ufanisi katika kulinda maslahi ya Taifa na kusimamia rasilimali za umma.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mafunzo ya Maafisa Sheria wa Serikali (State Attorney Training) ya mwaka wa fedha 2025/2026, yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026, Dkt. Possi alisema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa mawakili katika uendeshaji wa mashauri, usimamizi wa mikataba na utatuzi wa migogoro.
Alisema Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa kisheria ili kuhakikisha kila hatua ya miradi ya umma inalindwa kwa weledi na ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa mafunzo ya vitendo ikiwemo mazoezi ya kuiga kesi (trial simulation).
Dkt. Possi alitaja mafanikio ya mawakili wa serikali kuwa ni pamoja na kurejesha ndege ya Serikali iliyokuwa inashikiliwa nchini Afrika Kusini kutokana na madai ya mwekezaji, akisema ni uthibitisho wa weledi katika kulinda mali za Taifa nje ya mipaka.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo yanawakutanisha mawakili kutoka Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na taasisi za umma, kwa lengo la kuimarisha mshikamano na utendaji wa pamoja.
Kwa ujumla, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha utawala wa sheria, kulinda rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika huduma za kisheria nchini.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Bavoo Junus, alisema mawakili wa serikali wako tayari kikamilifu kulinda na kutetea maslahi mapana ya taifa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alisema mafunzo yanayotolewa ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi na weledi katika usimamizi wa mashauri ya serikali.
“Ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, watungaji wa sheria na mawakili wa serikali ni nguzo muhimu katika kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa manufaa ya taifa na wananchi,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, alisema mawakili wa serikali wana jukumu la msingi la kulinda maslahi ya taifa kupitia uandishi, uchambuzi na utekelezaji wa sheria kwa weledi na uadilifu.
Alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha ongezeko la upotoshaji wa taarifa, hususan mitandaoni, wataalamu wa sheria wanapaswa kuwa imara kuhakikisha sheria zinatekelezwa ipasavyo ili kulinda amani, ukweli na ustawi wa jamii.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, aliipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mkutano wa wadau wa sekta ya sheria, akisema ushirikiano wa taasisi hizo ni msingi muhimu wa utoaji haki.
Alisema Mahakama kama chombo cha mwisho cha utoaji wa haki inahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi zote za sheria ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Mahakama ni chombo cha mwisho katika utoaji wa maamuzi ya haki kwa wananchi, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi zote za sheria kushirikiana kwa karibu,” alisema.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shaban Abdalah, alisema mawakili wa serikali wanapaswa kuendelea kuonesha uzalendo, weledi na mshikamano katika kusimamia sheria na kulinda maslahi ya taifa.
Alisema serikali zote mbili zimekuwa zikitoa maelekezo ya mara kwa mara kuhusu kuimarishwa kwa mifumo ya sheria na matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro.
Alibainisha kuwa maelekezo hayo yanatolewa na viongozi wakuu, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambao wameendelea kusisitiza uwajibikaji na ufanisi katika taasisi za serikali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa huo, dkt Toba Nguvilla, alisema mawakili wa serikali wanapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuimarisha utawala bora na utoaji wa haki.
Alisema mafunzo hayo ni muhimu katika kipindi ambacho serikali inaendelea kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo, uwekezaji na utoaji huduma kwa wananchi.
Alisema kaulimbiu ya mafunzo hayo, “Litigate, Arbitrate, Serve the State, Serve the Future”, imebeba ujumbe wa kuwataka mawakili wa serikali kuitumikia nchi kwa weledi na uwajibikaji wa hali ya juu.
“Serikali inawategemea sana mawakili wake katika kutoa ushauri sahihi wa kisheria kwa viongozi na taasisi mbalimbali za umma,” alisema.
Aliongeza kuwa uandishi bora wa sheria na nyaraka za kisheria ni muhimu ili kuepuka migogoro inayotokana na tafsiri tata za sheria.
Aidha, alisema Arusha inaendelea kuwa kitovu cha mikutano ya kimataifa na uwekezaji, huku ikijiandaa kwa matukio makubwa kama Mkutano wa Mabunge Duniani (IPU) na AFCON 2027, hali inayoongeza umuhimu wa wataalamu wa sheria katika kuhakikisha mazingira salama ya kisheria.
Ends...











0 Comments