SERIKALI YAOKOA SHILINGI BILIONI 316 KUPITIA USHINDI WA MASHAURI 565 MAHAKAMANI

SERIKALI YAOKOA SHILINGI BILIONI 316 KUPITIA USHINDI WA MASHAURI 565 MAHAKAMANI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Dkt Ally Possi amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kushinda mashauri 565 kati ya mashauri 641 ya madai yaliyowasilishwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, sawa na wastani wa asilimia 88.1, hatua iliyosaidia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 316 ambazo zingelipwa na serikali kama fidia na madai mbalimbali.


Dkt Possi alitoa kauli hiyo jijini Arusha wakati akifungua mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo mawakili wa serikali, akisema mafanikio hayo yanaonesha namna serikali ilivyoendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria pamoja na kulinda maslahi ya taifa kupitia usimamizi madhubuti wa mashauri ya serikali.


Alisema pamoja na ushindi huo mkubwa mahakamani, serikali imeendelea kusisitiza matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro ili kupunguza gharama na muda wa usikilizaji wa mashauri mahakamani, hatua inayochangia kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.


Aidha, alisema katika kipindi hicho serikali ililipa zaidi ya Sh bilioni sita kwa ajili ya fidia na utekelezaji wa maamuzi ya mashauri mbalimbali yaliyokuwa yameamuliwa na mahakama.


Dkt Possi alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa mashauri kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwemo mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa mashauri, unaolenga kuongeza uwazi, kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma za kisheria nchini.


Alieleza kuwa serikali pia imeendelea kuwekeza katika mafunzo kwa mawakili wa serikali ili kuongeza uwezo wa kitaaluma katika utetezi wa maslahi ya taifa na kuhakikisha watumishi hao wanaendana na mabadiliko ya sheria na teknolojia.


“Tunajivunia kuona kuwa taaluma, uzalendo na mifumo bora ya sheria vinaendelea kusaidia kulinda rasilimali na maslahi ya nchi,” alisema Dkt Possi.


Kwa mujibu wake, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa wastani hushughulikia kati ya mashauri 100 hadi 200 kila wiki, jambo linaloonesha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kisheria serikalini pamoja na wajibu mkubwa unaoibeba ofisi hiyo.


Aliongeza kuwa serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, maktaba za kisasa za sheria pamoja na ushirikiano wa kimataifa katika kubadilishana uzoefu na taarifa za kitaaluma kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa mawakili wa serikali nchini.


Ends

Post a Comment

0 Comments